MTANGAZAJI

WATANZANIA HOUSTON WAPINGA SUALA LA HADHI MAALUM KWA DIASPORA

 

 
Watanzania waishio Houston,Texas Marekani wamemweleza Balozi wa Tanzania nchini Marekani na Mexico Elsie Sia Kanza kuwa hawakubaliani na pendekezo la  kupewa hadhi maalum kwa Diaspora isipokuwa wanahitaji mchakato wa Uraia pacha . 
 
 Wakizungumza mbele ya Balozi Kanza kwenye kikao kilichofanyika Houston Disemba 4,2021 pia wamemweleza kutoridhishwa kwao na utendaji kazi wa baadhi ya maofisa wa Ubalozi wa Tanzania nchini Marekani wanapowasilisha shida zao kwa ofisi hizo zilizoko Washington DC.
 
Akichangia hoja katika kikao hicho cha kwanza na Balozi huyo tangu ateuliwe, Erasto Mvungi amesema kuna jumuia kadhaa ikiwemo DAICOTA ambazo zimekuwa zikiwasiliana na baadhi ya viongozi serikali na zinaonekana kukubalina na suala la hadhi maalum kwa Daispora jambo ambalo sio sahihi kwani jumuia hizo haziwakirishi maoni rasmi ya wana Diaspora bali zina malengo ya maslahi binafsi.

Steven Maonyesho amesema yeye ni raia wa Tanzania kwa kuzaliwa haelewi sababu hasa ya kumfanya apewe hadhi maalum wakati ni mtanzania ambaye anaweza kuwekeza Tanzania, na hadhi maalum haipo kikatiba hivyo suala hilo anaona limekaa kisiasa na sio kwa maslahi mapana kwa watanzania walioko nje ya Tanzania.

Pia watanzania hao walimweleza Balozi kuwa baadhi ya maafisa wa Ubalozi wa Marekani waliopo Washington DC wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa weledi katika kuwahudumia vizuri wateja wao ambao miongoni mwao ni watanzania.

"Wafanyakazi wa Ubalozi wanapaswa kufahamu kuwa wanafanya kazi wakiwa Marekani, wanatakiwa kuwa na huduma nzuri kwa wateja hata kama mteja ameulizia jambo ambalo kwao linaonekana halina maana"amesema Sule Kisaka.

Balozi Kanza amesema maoni yaliyotolewa na watanzania hao ni ya msingi na yanahitaji utekezaji wake,Balozi huyo anatembelea majimbo mbalimbali nchini Marekani  kwa lengo la kukutana na watanzania.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.