MTANGAZAJI

WASIWASI WA KUTOWEKA KWA ZIWA JIPE

 

 Serikali ya Tanzania imeeleza wasiwasi wa kutoweka kwa Ziwa Jipe wilayani Mwanga Mkoa wa Kilimanjaro kutokana na uwepo wa magugu maji yaliyozingira Ziwa hilo.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira)nchini Tanzania ,Hamad Hassan Chande Chande ameeleza wasiwasi huo Septemba 20,2021  alipofanyaziara ya kikazi kukagua athari za kuenea kwa magugu maji hayo katika Ziwa Jipe ambapo amewataka wataalamu wa mazingira kufika katika Ziwa hilo na kufanya upembuzi yakinifu utakaosaidia kuyaondoa magugu maji yaliyozingira ziwa hilo.
 
Akizungumza wakati wa ziara hiyo alitahadharisha kuwa kutoweka kwa ziwa hilo
kunaweza kusababisha madhara makubwa kwa Taifa la Tanzania kwani wananchi
wanaweza wakapoteza fursa za uwekezaji.
 
“Nimejionea madhara ya magugu maji katika ziwa hili jambo ambalo linaweza
kusababisha likapotea kabisa katika ramani hivyo naelekeza wataalamu wetu wa
mazingira wajiridhishe kabla ya kuomba fedha kutoka kwa wahisani wa ndani na
nje watusaidie fedha ili kuondoa magugu haya,” alisema.
 
Kutokana na changamoto ya kutofanyika kilimo endelevu, Chande aliutaka Uongozi wa Wilaya ya Mwanga pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama kuhakikisha wanadhibiti kilimo kisicho endelevu kando ya ziwa ambacho husababisha athari za kimazingira ikiwemo mmomonyoko wa udongo.
 
Katika kuhakikisha mipaka ya ziwa hilo inalindwa aliwahakikishia wananchi kuwa
suala hilo litafanyiwa kazi kwa kuhusisha nchi zote mbili yaani Tanzania na
Kenya ili Watanzania wafaidi rasilimali zao.
 
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mwanga,  Joseph Tadayo aliiomba
Serikali kutatua changamoto hiyo kwa kuondoa magugu hayo ndani ya ziwa
akisema kuwa linategemewa kwa shughuli mbalimbali zikiwemo uvuvi, mradi
mkubwa wa maji wa Same, Mwanga na Korogwe pamoja na kilimo cha
umwagiliaji.
Tadayo alisema ziwa hilo litasaidia kuongeza ajira hususan kwa vijana na hivyo
kunufaisha wakazi takriban 2,564 wanaolizunguka pamoja na baadhi ya
wananchi wa Wilaya jirani ya Moshi Vijijini.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.