MTANGAZAJI

MFUMO WA UKAGUZI WA MIFUGO TANZANIA

 

 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi nchini Tanzania  Mashimba Ndaki amezindua mfumo wa ukaguzi wa mifugo na mazao yake na kuwataka watakaotekeleza mfumo huo kutogeuka kuwa Jeshi la Polisi na watoa hukumu kwa wananchi.

 
Ndaki ametoa kauli hiyo hivi karibuni  jijini Dodoma, wakati wa uzinduzi wa mfumo huo ili kuongeza tija na kuinua pato la taifa kupitia sekta ya mifugo.
 
Amesema mfumo huo ni rahisi na ushirikishwaji hivyo ni vyema wakaguzi kutogeuka kuwa Jeshi la Polisi na kuwasumbua wadau wa sekta ya mifungo.
 
Ameongeza kuwa umuhimu wa mfumo huo ni kuhakikisha utekelezaji wa wajibu wa kulinda afya za walaji, mifugo na mazao yake kwa kusimamia sheria, kanuni na taratibu jambo ambalo litasaidia wafugaji kuzalisha mifugo kwa tija kwa kutumia pembejeo na huduma zilizosajiliwa na kutambuliwa kisheria.
 
Ametoa rai kwa wakaguzi kutumia mfumo wa ukaguzi wa mifugo na mazao yake kuhakikisha sheria, kanuni, taratibu za kusimamia na udhibiti wa ubora, usalama na viwango stahiki vinasimamiwa na kutekelezwa ipasavyo.
 
Waziri Ndaki amewaomba wafugaji wote nchini kujenga utamaduni wa kutumia pembejeo na malighafi zenye ubora, usalama, viwango stahiki kutoka kwenye vyanzo vilivyosajiliwa kwenye uzalishaji wa mifugo.
 
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Miugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo, Bw. Amosy Zephania amesema wizara imeanzisha na kuboresha mfumo wa ukaguzi wa mifugo na mazao yake ambao umejikita kwenye tasnia za kuku, maziwa, nyama, mayai, ngozi, malisho na rasilimali za vyakula vya mifugo.
 
Amebainisha kuwa mfumo huo umeanishwa kwa kushirikiana na Benki ya Dunia kupitia mradi wa maboresho ya ufugaji kibiashara (L-MIRA) ambao umewezesha kufanyika mapitio ya sheria tatu za Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Wanyama ya mwaka 2010, Magonjwa ya Wanyama ya mwaka 2003 na Sheria ya Veterinari ya mwaka 2003 na kanuni 12.
 

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.