UADILIFU WATAKIWA KUWEZESHA UCHUMI WA BLUE
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Zanzibar, Haroun Ali Suleiman, amewataka watakaopewa jukumu la kuendesha Boti iliyotolewa kwa Taasisi ya Mfuko wa Maendeleo ya Elimu Jimbo la Kikwajuni kwa ajili shuguli za uchumi wa blue kuwa waaminifu ili kutimiza lengo lililokusudiwa.
Waziri Suleimani ametoa rai hiyo kwa niaba ya
Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, wakati wa
kukabidhi zawadi kwa washindi wa Shindano la Kuhifadhi Quran pamoja na
kukabidhi Boti kwa Taasisi ya Mfuko wa Maendeleo ya elimu Jimbo la Kikwajuni,
yaliyoandaliwa na kutolewa na Naibu Waziri Fedha na Mipango, na Mbunge wa jimbo
hilo, Mhandisi Hamad Yussuf Masauni.
Alisema kuwa bila kuwa na uaminifu katika matumizi ya
Boti, hakutakuwa na tija la boti hiyo, hivyo kudidimiza lengo la Taasisi ya Mfuko
wa Maendeleo ya Jimbo la kuwapatia ajira vijana kupitia Boti litakalotumika
katika shughuli za uvuvi.
“Nimewahi toa Boti mbili tatu kwa ajili ya uvuvi
lakini kila nikihitaji kupata mrejesho naambiwa leo baharini hakuingiliki au
Samaki hawapatikani, wakati napata taarifa kwa wengine kuwa Samaki wamepatikana,
kama hakutakuwa na vijana waaminifu basi mradi huo hautaendelea”, alieleza Mhe.
Waziri Suleiman.
Aidha amewataka vijana kujiepusha na vitendo vya
utumiaji dawa za kulevya, uzalilishaji na kukosa uaminifu ili miradi hiyo
iliyobuniwa iweze kutekelezeka na kuwanufaisha vijana na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Fedha na Mipango ambaye
ni Mbunge wa jimbo la kikwajuni, Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, amesema
kuwa Serikali imekuwa ikiweka miundombunu wezeshi kwa wananchi, lakini kutokana
na kukosekana kwa uaminifu miundombinu huharibiwa na miradi kufa, hivyo ameamua
kutoa Boti kwa Taasisi Mfuko wa Maendeleo ya Elimu Kikwajuni ambayo inasimamiwa
na watu wenye Imani ya Dini ili kukomesha ubadhirifu na kuleta tija stahiki.
Mheshimiwa Mhandisi Masauni amebainisha kuwa Boti na
Mashine inathamani ya ya zaidi ya Shilingi milioni 15 na ameikabidhi Taasisi hiyo pamoja na Shilingi milioni tano
ya mradi wa Majongoo Bahari, ili kutekeleza lengo la Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar la kuwekeza nguvu kwenye uchumi wa Blue.
“Taasisi ya Mfuko wa Maendeleo ya Elimu Jimbo la
Kikwajuni imekuwa na shughuli nyingi za kutatua changamoto za elimu kwa kufadhiliwa
na watu binafsi kwa ruzuku, kwa kuwa
Serikali inayonia thabiti ya kuhakikisha wananchi wanajikwamua kiuchumi,
tumeamua kuifanya taasisi hiyo iweze kujiendesha kwa kiasi kikubwa kwa kutumia
miradi yake yenyewe”, alieleza Mhandisi Masauni.
Post a Comment