MTANGAZAJI

TANZANIA KINARA WA UBORA WA SEKTA YA FEDHA KUSINI MWA AFRIKA

 

Imeelezwa kuwa sekta ya Fedha nchini Tanzania inaongoza kwa uimara na ubora katika nchi za Kusini mwa Bara la Afrika na Afrika Mashariki kwa vigezo vyote kutokana na usimamizi madhubuti wa uchumi na maboresho ya sekta hiyo.

Hayo yamebainishwa na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Prof. FLorens Luoga, wakati wa Semina kuhusu masula ya Fedha na uchumi kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, iliyofanyika Zanzibar.
Prof. Luoga alisema kuwa Benki Kuu inajivunia mafanikio makubwa katika mageuzi na maboresho ya Sekta ya Fedha ambayo yameifanya Sekta kuwa tulivu na kuwafanya wawekezaji kuwa na Imani zaidi ya kuwekeza nchini.
“Kutokana na uimara wa Sekta ya Fedha,Tanzania inashika nafasi ya tatu Barani Afrika kwa vigezo vya kukopesheka ikitanguliwa na Nigeria na Ethiopia na haya ni matokeo ya usimamizi thabiti wa uchumi wa nchi”, alieleza Prof. Luoga.
Alisema katika kutekeleza majukumu ya usimamizi wa sekta ya fedha, kuna umuhimu wa kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja na wadau, wakiwemo Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar ili kufikia malengo yanayopangwa hususani katika kufanikisha ukuaji, utulivu na ustawi endelevu wa sekta ya fedha na uchumi.
Alisema kuwa Benki Kuu ya Tanzania  inayo adhma ya kuendelea kutekeleza majukumu yake makuu ya kudumisha mfumo madhubuti na salama wa fedha na mabenki kwa kupitia usimamizi makini wa mfumo wa malipo wenye usalama na unaoenda na wakati.
Aidha alisema kuwa Semina kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi inalengo la kuwajengea uelewa mpana juu ya majukumu ya BoT pamoja na masuala ya masoko ya fedha hususani Dhamana na Hati Fungani za Serikali.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Fedha na Mipango,Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, alisema kuwa BoT, imefanya tafiti takribani tatu kuhusiana na uchumi wa Blue hivyo ni fursa kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuchangia mawazo katika eneo hilo ili kuwezesha kutoa mchango kwa Serikali kwa adhma ya kukuza uchumi na kupunguza umasikini.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.