WATENDAJI WA SHIRIKA LA POSTA TANZANIA WATAKIWA KUWA WATENDAJI WANAOACHA ALAMA
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Dkt.Zainabu Chaula ametaka Meneja wakuu, Meneja wa mikoa yote na wakuu wa idara wa Shirika la Posta Tanzania (TPC) kutumia nafasi zao, maarifa na utaalamu wao wote kuhakikisha wanalitendea haki Shirika la Posta Tanzania na utendaji wao uache alama.
Dkt. Chaula ameyazungumza hayo alipokuwa anafungua mafunzo ya siku tano ya uwajibikaji kwa kufuata sheria na taratibu za utumishi wa umma kwa meneja wakuu, wakuu wa idara na meneja wa mikoa yote wa TPC yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa TBA, jijini Dodoma.
Ameongeza kuwa kila mtumishi anatakiwa ajiwekee malengo na kujitathimini kulingana na majukumu aliyokabidhiwa ambapo kufanikisha hili ni lazima kufanya kazi kwa kushirikiana,kusaidiana na kuwezeshana kwani mashindano maofisini hayajengi ,njia pekee ya mafanikio ni kuzifanyia kazi changamoto kwa kuzitafutia ufumbuzi.
Postamasta Mkuu Hassan Mwang’ombe amesema kuwa Shirika la Posta limeendelea kupanua wigo wa huduma zake ambapo kwasasa Shirika limejiingiza zaidi kwenye biashara ya uwakala wa huduma mbalimbali ili mteja akifika kwenye dirisha la posta aweze kupata huduma nyingine muhimu kama vile huduma za kibenki, bima na intaneti kwa kupitia telecentres zinazojengwa na Shirika hilo.
Akiongelea mafunzo hayo Mwang’ombe amesema kuwa lengo kubwa ni kukumbushana nakuelekezana katika kutimiza majukumu na uwajibikaji ili Shirika liweze kupata matokeo chanya.
Post a Comment