MTANGAZAJI

WATENDAJI POSTA WATAKIWA KUWA WABUNIFU

 

Msajili wa Hazina Athumani Selemani Mbutuka akizungumza wakati akifunga mafunzo ya
siku tano ya watendaji wakuu wa Shirika la Posta Tanzania (TPC) yaliyofanyika katika Ukumbi
wa TBA, jijini Dodoma, wa Kwanza aliyeketi kulia ni Postamasta Mkuu wa TPC, Hassan
Mwang’ombe akifuatiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya TPC Kanali Mstaafu Dkt. Haruni Kondo.


Msajili wa Hazina Athumani Selemani Mbutuka (walioketi katikati) akiwa kwenye picha ya
pamoja na viongozi wakuu wa Shirika la Posta Tanzania (TPC) kushoto walioketi ni
Postamasta Mkuu wa TPC, Hassan Mwang’ombe akifuatiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya TPC
Kanali Mstaafu Dkt. Haruni Kondo na Kulia walioketi ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya
Mawasiliano Caroline Kanuti wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya
Mawasilano) akifuatiwa na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu wa Wizara hiyo,
Kitolina Kippa.

Msajili wa Hazina Athumani Selemani Mbutuka ameliagiza Shirika la Posta Tanzania(TPC) kubadilika katika utendaji wao kulingana na ushindani uliopo na mashirika mengine, kwa kuwa wabunifu kibiashara na kuweka malengo ya kuongeza ukusanyaji wa mapato hasa katika biashara yake ya duka la kubadilisha fedha (Bureau de change) ili kuhakikisha wanaongeza uzalishaji, na uchumi wa Shirika hilo unaimarika ili kuweze kutoa gawio kubwa kwa Serikali.


Mbutuka ametoa agizo hilo alipokuwa akifunga mafunzo ya siku tano ya viongozi
wakuu wa Shirika hilo yaliyofanyika katika ukumbi wa TBA jijini Dodoma.


“Ili uingine katika ushindani ni lazima uwe na uwezo wa kushindana kwa kuzingatia fursa zilizopo, mahitaji ya wateja na ukuaji wa teknolojia, hasa kipindi hiki cha matumizi ya TEHAMA katika kutoa huduma mbalimbali kwa jamii. Shirika hili limepewa dhamana ya kutoa huduma nyeti na muhimu kwa Serikali na jamii, hivyo linatakiwa kuwa Shirika la mfano na lijiendeshe kwa faida kwa kuhakikisha kila tawi la Posta nchini linatoa huduma bora na kuzalisha faida kwa Shirika na kuweza kutoa gawio kubwa zaidi kwa Serikali”, alizungumza Mbutuka.


Aliongeza kuwa mafunzo waliopata viongozi wakuu wa Shirika hilo ni mtaji mzuri kwa viongozi na yapelekwe kwa wafanyakazi walio chini yao ili kuboresha utendaji,kuongeza uzalishaji, ufanisi na ubunifu katika kutoa huduma kwa jamii na kutimiza malengo ambayo Shirika limejiwekea ya kujiimarisha kiutendaji na kiuchumi.


Mwenyekiti wa Bodi ya TPC Kanali Mstaafu Dkt. Haruni Kondo ametoa rai kwa watendaji wa Shirika hilo kushikana pamoja na kufanya kazi kwa bidii ili kulinda nafasi zao na kuikusanyia Serikali mapato stahiki kwa kuacha kufanya kazi kwa mazoea katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya Shirika hilo la kuhudumia wananchi na Serikali. 


Naye Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano) Kitolina Kippa akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo amewataka Meneja wa Mikoa na Kanda wa Shirika hilo kuboresha mahusiano mahala pa kazi kwa kuheshimu mamlaka zilizo juu yao ili na watendaji walio chini yao wawaheshimu na kuepusha migogoro ambayo inapunguza utendaji wa kazi na uzalishaji.

Postamasta Mkuu wa TPC Hassan Mwang’ombe amesema kuwa Shirika hilo sasa lipo katika harakati za kuanza kutoa huduma kidigitali na tayari limekwishandaa mfumo maalumu wa kutolea huduma unaoitwa Postal Management Information System (PMIS) na huduma za Posta zitaingizwa ndani ya mfumo huo, ambapo mpaka sasa mfumo wa malipo wa MUSE, EMS na barua tayari vimeshaingizwa katika mfumo huo.


Katika hatua nyingine Mwang’ombe amempongeza Meneja wa TPC Mkoa wa Mtwara kwa ubunifu wa kuleta wazo la Shirika hilo kuwa Wakala wa huduma za kibenki na Benki ya watu wa Zanzibar (PBZ), ambapo tayari uzinduzi wa ushirika huo umekwishafanyika na kwa kuanzia huduma za PBZ zitaanza kutolewa na TPC katika mikoa nane Tanzania bara na baadae nchi nzima. Aidha, alitumia fursa hiyo kuwaasa Meneja wake kuwa wabunifu katika kutoa huduma za Posta nchini.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.