MTANGAZAJI

WHO KUSHIRIKIANA NA WAADVENTISTA WA SABATO KUPUNGUZA VIFO VYA AKINA MAMA NA WATOTO
Shirika la Afya Duniani (WH0) na Kanisa la Waadventista Wa Sabato wameingia katika ushirikiano wa  mkakati wa kiulimwengu  katika kupunguza vifo vya watoto na akina mama wakati wa kujifungua.

Annette Mwansa Nkowane afisa toka WHO anaeleza kuwa hii ni mara ya kwanza kwa shirika hilo linajihusisha na masuala ya afya  kuingia ubia na taasisi ya dini  katika mkakati wa miaka mitano kutoa mafunzo kwa wakunga.

Viongozi wa wauguzi na wakufunzi 50 toka Amerika ya Kaskazini,Ulaya,Amerika ya Kusini na Afrika juma hili wamekutana katika mji wa Bloemfontein, Afrika ya Kusini kwa ajili ya kuzindua mradi huo ambao utaanza kutekelezwa katika nchi nne za Afrika.

Mradi huo ambao utagharimu dola milioni 1 za kimarekani umedhaminiwa na mradi wa maendeleo wa kimataifa OPEC kupitia WHO na kuratibiwa na viongozi wa shirika hilo na wale wa Kanisa la Waadventista Wa Sabato duniani kupitia Chuo kikuu cha utabibu cha Loma Linda.

Kwa mujibu wa takwimu za WHO kiasi cha akina mama wajawazito 280,000 hufariki wanapojifungua kila mwaka duniani huku ikielezwa kuwa Afrika ina asilimia 12 ya madaktari na wakunga asilimia 30 ambapo idadi hiyo ni ndogo kutokana na ongezeko la watu barani humo kwani hitaji ni kufundisha asilimia kumi hadi 30 ya madaktari.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.