MTANGAZAJI

MARA:MWANAMKE ALIYECHOMWA MOTO SEHEMU ZA SIRI NA MUMEWE AHOFIA USALAMA WAKE



Mwanamke aliyechomwa moto sehemu za siri na mumuwe mwezi wa saba mwaka huu, anaishi kwa hofu kutokana na mumewe kudaiwa kuonekana kijijini Murito akiwa na panga lenye makali baada ya mama mkwe  na wifi yake kumfuata nyumbani kwao naye kuwakatalia kurudi kwa mume huyo.

Akizungumza leo  nyumbani kwao katika kitongoji cha Nyambeho kijiji cha Murito, Wilayani Tarime Agines Marwa 18 amesema kuwa ameingiwa na wasiwasi mkubwa hivyo hulazimika kutembea akiwa ameambatana  na mama yake mzazi kwa kuhofia kudhuriwa akiwa peke yake.

Agines amesema kuwa ujauzito wake umetimiza miezi saba na anamwomba Mungu ajifungue mtoto wake salama, kwa kuwa wakati anaondoka katika kituo cha afya Nyamongo alikokuwa amelazwa Daktari alimweleza kuwa atajifungua salama kwani hakupata madhara makubwa.

Hata hivyo mama yake Nsato Marwa amesema kuwa, kwa sasa wanasubiri waone kama binti yao atajifungua salama kutokana na majeraha aliyopata ndipo waweze kuzungumzia uamuzi wa kufanya lakini mpaka sasa kama familia hawana neno lolote la kufanya.

Agines Marwa alichomwa moto na mume wake mwezi wa saba mwaka huu baada ya kukutwa na shilingi 2000 kwenye pochi yake na mume wake kumtuhumu kuhongwa na wanaume kiasi hicho cha pesa, licha ya kumpiga na kumfunga kwa kamba nje akinyeshewa na mvua, Mume huyo aliamua kumchoma sehemu zake za siri kwa kijinga cha moto.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.