MTANGAZAJI

DODOMA:KATIBA PENDEKEZWA YA TANZANIA YAKABIDHIWA KWA VIONGOZI WA SERIKALI YA NCHI HIYO



Mwenyekiti wa Bunge la Katiba  inayopendekezwa Mh Samweli Sita amekabidhi katiba hiyo kwa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dr Jakaya Mrisho Kikwete na Raisi wa Zanzibar Dr Ally Mohamed  hii leo katika uwanja wa jamhuri jijini Dodoma.

Akizungumza katika sherehe za kukabidhiwa katiba hiyo zilizoanza saa 6:00 mchana hadi saa 2:25 leo usiku  huko Dodoma,Rais Kikwete amesisitiza katiba inayopendekezwa haitatumika katika uchaguzi ujao labda kama kutafanyika maamuzi mengine ingawa hatarajii maamuzi hayo yatokee.

Amesema katiba hiyo inaunganisha makundi yote na kuwafanya wananchi wajisikie kuwa haki zao zinazingatiwa na kuwa inaonesha umoja upendo na mshikamano kwa watanzania na kustawisha demokrasia na utawala bora na akasisitiza kuwa ina mambo mazuri kwa maslahi ya taifa na inakwenda na wakati kwa kuwa ina gusa makundi yote.


Sherehe  hiyo hii leo ilihudhuriwa na  marais wastaafu wa Zanzibar na Tanzania Bara,mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao nchini , viongozi wa ngazi tofauti wa kitaifa, watu mashuhuri na wawakilishi wa makundi yote ya jamii ya Watanzania, ambayo yameguswa na katiba hiyo inayopendekezwa.

Oktoba 2 mwaka huu Bunge maalumu la Katiba nchini Tanzania lilipitisha rasimu ya katiba iliyopendekezwa,hatua hiyo ilifikiwa baada ya kura za ndio zilizopigwa na wajumbe kufikia kiwango kinachostahili, ili katiba hiyo iliyopendekezwa ipite ilitakiwa kuungwa mkono na kura za ndio theluthi mbili kutoka Tanzania bara na theluthi mbili za ndio kutoka Zanzibar.

Rasimu hiyo ya katiba ilipendekezwa na kamati ya uandishi kuwa na jina la KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA YA MWAKA 2014 .


 
Hata hivyo sherehe hizo hazijahudhuriwa na viongozi wa vyama vya upinzani nchini kwa madai kuwa mapendekezo ya katiba hiyo hayajazingatia maslahi ya taifa.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.