MWAKA MMOJA JELA KWA KOSA LA KUMSHAMBULIA MKEWE KWA PANGA NA FIMBO
Amosi Samwel Nkororo akiingia kwenye gari la polisi amefungwa pingu kwenda kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela(Picha na WaitaraMeng’anyi) |
Amosi Samwel Nkororo 38 mkazi wa kijiji cha Sirari kata ya
Sirari tarafa ya Inchugu Wilaya ya
Tarime amehukumiwa mwaka mmoja jela kwa kosa la kumshambulia mkewe kwa panga na fimbo na kumsababishia majeraha kichwani Wilayani hapa.
Aliutenda unyama huo juni moja saa 11 jioni alipoingia nyumbani na kuanza
kumshabulia mkewe aitwaye Mariam Daniel 34 kwa panga akimtuhum u kulala nje ya
familia bila taarifa ama ruhusa yake.
“Nilipigiwa simu jana
yake siku ya tarehe 31 kuwa mama mzazi anaumwa nikaamua kukimbia kwenda
kumwaona kwa kuwa ni mtu mzima huko Magoto, nililala na kesho yake saa tatu
asubuhi nilikuwa kwangu maana niliwaacha watoto wadogo” alisema Mariamu.
Mariamu Daniel miaka 34 aliondoka na kuripoti kituo cha
polisi sirari na kupewa kibali cha kutibiwa akiwa amekimbia mji kwa kuwa
Nkororo alikuwa akimtafuta kwa kile kilichodaiwa
kuwa alitaka kumwondoa uhai huku akidai kuwa muke hawezi kumiliki hati ya
Nyumba waliojenga
Mariamu ameeleza kuwa wameishi pamoja kwa muda wa miaka
mitano na katika muda huo walikuwa
wakiishi vizuri japo Nkororo alikuwa akimfanyia ukatili kwa kumpiga jambo ambalo
alilichukulia kuwa ni la kawaida.
Baada ya kuona hali ya maisha ya mumewe si nzuri kwa kuwa ni
msukuma toroli Mariamu aliamua kwenda kwenye kikundi kukopa shilingi laki tano kumletea mumewe aweze kuwa anachukuwa
machungwa kutoka Musoma na kuyauza
ili kuongeza kipato katika
familia yao, huku akimpa shilingi elfu
20 kila mwezi kurudisha katika kikundi chake.
Mariamu ameeleza kuwa fedha hizo zilitumika kwa starehe na
hazikuleta faida yoyote zaida ya kuwa analeta wanawake nyumbani huku akinoa
panga na kisu akimtishia kuwa atamchinja
kwani yeye ni mtu kuja akimaanisha si mzaliwa wa Sirari.
“Shida ilianza baada ya kununua uwanja na kuanza kujenga hii
nyumba alianza kuniambia nimpe barua ya mkataba wa kununulia ploti hii, na
alipoona sifanyi anavyotaka akaanza kujaribu kujinyonga nyakati za usiku wakati
Fulani akichora ramani ya kaburi hapo uani akisema hapa ndipo nitakapo zikwa
nikifa” alisema . Mariamu Daniel.
Kutokana na kipigo hicho cha mwezi juni mariamu aliamua
kwenda kwa sheria kutafuta usaidizi.
Chini ya mwongozo wa kituo cha SHEHABITA
aliifikisha kesi hiyo mahakama ya mwanzo ya Sirari na kuamua
kuisimamia kwa kipindi chote cha miezi
sita.
Hata hivyo Bi Mariamu anaonekana msaliti wa mila na desturi
kwa kumshitaki mumewe na kuhukumiwa kifungo cha mwaka mmoja.
“Wanawake wenzangu wananishangaa wananiuliza hivi kweli
umemfunga mume wako si utaharibu mahusiano yako na wakwe zako?” alieleza
Hata hiyo wakazi na mashuhuda wa hukumu hiyo ambayo ni ya
kwanza kufikia hukumu wamshukuru bi Mariam kuwa jasiri na kusimamia kesi yake
hadi mwisho maana waengi huzifungua kesi za namna hiyo na baadaye kutoroka
hazijafikia hukumu.
“sikutumia hata senti moja katika kesi hii bali ni maelezo
yangu na ushahidi wa mwanagu Shadrack Mwita 10 alioutoa nimetendewa haki japo
adhabu aliyopewa bado mimi naona ni ndogo kutokana na maumivu aliyonisababishia
kichwani” alisema .
Akisoma hukumu katika
mahakama ya mwanzo Sirari Hakimu Bi, Pestaflora Chacha alieleza kuwa mnamo
tarehe moja ya mwezi wa sita mwaka Nkororo alimshambulia mkewe kwa panga kwa
kumkata majeraha mawili kichwani na kumsababishia maumivu makali yaliyomsababisha
kulazwa na kushonwa nyuzi 8 kwa jeraha la kwanza na nyuzi 6 kwa jeraha la pili.
Nkororo aliiomba mahakama ipunguzie adhabu kwa kuwa
anategemewa na familia na kubadilishiwa adhabu ili apewe kifungo cha nje
angalau cha kufagia na kufanya usafi eneo la mahakama hiyo ya mwamzo.
“Adhabu uliyopewa ni ndogo kulingana na kosa ulilolifanya,
na ni kwa kuwa Mahakama hii ina uwezo wa kutoa
adhabu ya kiwango hicho hata hivyo nakutuma mahakama ya Wilaya ili
hukumu yako ipitiwe ikionekana nimekuonea watakupunguzia na ikionekana
nimekuhurumia itajuwa cha kufanya” alisema Hakimu Bi, Pestaflora.
Hata hivyo Hakimu Pestaflora akitoa hukumu hiyo amesema,
kutokana na kitendo cha Nkororo kumshambulia mkewe kwa kudai kuwa alikuwa
akimrudi ambacho ni kinyume cha sheria
ya ndoa namba 5 ya mwaka 1971 kifungu cha 66 kinachosema si mume wala mke atakayerusiwa kumpiga
mwenzake kwa kosa liwalo lote amemhukumu kifungo cha mwaka mmoja jela kulingana
kiwango cha adhabu inayoruhusiwa kisheria kutolewa na mahakama ya mwanzo japo
alistahili adhabu kubwa zaidi.
Aidha ametoa hukumu hiyo kuwa fundisho kwa wanaume wengine
wenye tabia mfumo dume waitumiayo
kutatua migogoro ya familia zao ambayo imepitwa na wakati.
Naye Mkurugenzi wa chama cha waandishi wanawake Tanzania TAMWA Bi Valerie
Msoka ameishukuru mahakama kwa kumtendea haki Bi Mariamu kwa kumhukumu mumewe
kutokana na ukatili aliounesha kwake, aidha ametoa rai kwa mahakama vyesi vya
ukatili vichukue muda mfupi kusikilizwa na kutolewa hukumu badala ya kuchukuwa
muda mrefu ili kuwafanya wakatiliwa kupata haki yao ya kisheria kwa wakati.
“Tunawaomba wanawake wote wanaofanyiwa unyanyasaji huu
popote wakaripoti katika vituo vya polisi na kupeleka kesi hizi mahakamani
kwani haki inatendwa wazisimamie hadi
mwisho wasiogope” alisema mkurugenzi huyo wa TAMWA.
Naye msaidizi wa sheria na haki za bindamu Bwn, Mrimi
Zabroni ameelea kufurahishwa kutokana na maamuzi yaliyofikiwa na mahakama hiyo
katika shauri namba 169 la mwaka 2013 kufikia hukumu.
“Hii ni kesi ya kwanza kutolewa hukumu tangu nianze kazi na
imenitia moyo kuendelea kuwasaidia wanaoonewa kwa kuwaonesha wapi haki yao
ilipo kwa kufuata sheria kwani sheria zipo na zinztekelezwa kwa kufuta misingi
ya nchi” alisema Zabron msaidizi wa sheria kutoka shirika la haki za binadamu
SHEHABITA
Imeandikwa na Waitara Meng'anyi toka Tarime
Post a Comment