MTANGAZAJI

WIZARA YA MAMBO YA NDANI NCHINI TANZANIA YAKANUSHA WAZIRI NCHIMBI KUPOPOLEWA


TAARIFA KWA UMMA

Habari iliyotolewa Oktoba 26, mwaka huu na baadhi ya magazeti na mitandao ya kijamii yenye kichwa cha habari ‘Msafara wa Waziri Nchimbi wapigwa mawe Songea’ si za kweli bali zimetengenezwa na walizituma kwa nia ya kupotosha jamii.

Oktoba 25, mwaka huu, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini, Dk. Emmanuel Nchimbi alitembelea Miradi ya Maendeleo pamoja na kufanya Mkutano aliianza katika Kata ya Mletele na kumalizia Kata ya

Matarawe, katika jimbo lake la Songea Mjini. Wakati alipomaliza mkutano wake wa Mletele alitaarifiwa makundi ya watu yamefunga njia katika daraja la Matarawe na wamesema hawatalifungua mpaka Mhe Nchimbi akaliangalie na kuzungumza nao.
Mhe. Nchimbi alishauriwa kubadili njia ili kuwahi mkutano wa hadhara wa Matarawe ambapo wananchi walikuwa wanamsubiri kwa zaidi ya saa mbili. Pamoja na kushauriwa kupita njia nyingine, Mhe. Nchimbi aliamua kwenda kuwasikiliza, alifika katika eneo la daraja akiwa amefuatana na viongozi mbalimbali wa Manispaa na Serikali, mhe Nchimbi aliwapa fursa wananchi hao kueleza kero zao, nao walimwambia kuwa eneo hilo limekuwa na ajali mara kwa mara tokea barabara ya lami ilipokamilika na kusababisha vifio vya watu karibu wanne hivyo walimuomba mbunge wao awasaidie kumaliza kero hiyo.

Akijibu kero hiyo, Mhe. Nchimbi aliwaambia wananchi wake kuwa ni yeye aliyefanikisha ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami atalishughukia tatizo hilo pia na kuwa amelichukua kwa uzito mkubwa. Baada ya majibu ya mhe Nchimbi wananchi hao waliridhika na ndipo wenyewe wakafungua barabara na kutoa vizuizi ili waziri na msafara wake waweze kupita. Mhe Nchimbi na ujumbe wake waliendelea na safari na kwenda kwenye mkutano wa hadahara takribani mita 200 toka daraja hilo. Saa moja baada ya mhe Nchimbi kuwa ameshapita baadhi ya vijana walifunga tena barabara na ndipo Jeshi la Polisi lilipolazimika kuwatawanya na kuwakama vijana saba.

Waandishi wa habari wa Televisheni za Star TV, Channel Ten na TBC wanamikanda ya tukio zima na hivyo mikanda hiyo inaweza kuthibitisha habari kuwa mhe Nchimbi alipigwa mawe ni uzushi mtupu.

Waziri Nchimbi alikuwa katika ziara ya kawaida jimboni kwake na aliweza kufanya mikutano minane ya hadhara iliyohudhuriwa na mamia ya watu na iliendeshwa kwa utulivu mkubwa ambapo wenyeviti wa mikutano hiyo walikuwa madiwani wa kata husika, ambapo katika kata sita mikutano hiyo iliongozwa na madiwani wa CCM na kata mbili iliongozwa na madiwani wa Chadema.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi inavisihi vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kujiridhisha na ukweli wa taarifa wanazozipata kabla ya kuzitoa kwa wananchi ili wananchi waweze kupata haki yao ya kupata habari zilizokuwa sahihi.

Mwisho.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
28 Oktoba, 2013

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.