SHIDA YA MAJI YAKIKUMBA CHUO CHA UALIMU TARIME,MARA
|
Chuo cha Ualimu Tarime kilichoko
Wilayani Tarime mkoani Mara kiko hatarini kukumbwa na magonjwa ya mlipuko
kutokana na uhaba wa maji uliopo katika chuo hicho unaosababishwa na
idadi kubwa ya wanachuo zaidi ya 800 walioko chuoni hapo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na
blog hii Wilayani humo, walisema kuwa wanahofia hali ya afya zao kutokana na
wingi wa wanachuo ambao hutumia bomba moja linalofanya kazi kwa nguvu ya
mashine ya kusukuma maji ambayo nayo kwa sasa haifanyi kazi kwa kuharibika.
“Tuna shida ya maji kutokana na
mashine inayosukuma maji kuharibika na sasa tunaloa maji kwa kutumia ndoo kwa
kupiga msitari na mara nyingi maji huisha bila sisi kuenea na kuamua kuingia
darasani bila kuoga” alisema mmoja wa wanachuo hao bila kutaka kujwa jina lake.
Kutokana na ratiba ya chuo hicho
kuwa finyu, wanachuo hulazimika kupewa muda mufupi wa kuchota maji na kuoga
ambapo hawaenei kutokana na idadi kubwa iliyopo kwa sasa kwa kuwa chuo hicho
kina uwezo wa kuchukuwa wanachuo 500 tu.
“Bweni la Kenyata lenye uwezo wa
kubeba wanachuo 105 kwa sasa linawachuo wapatao 180 huku lile la Nkurumah lenye
uwezo wa kubeba wanachuo 135 kwa sasa lina jumla ya wanachuo 200 kutokana
na uhaba wa mabweni” alisema mwanachuo huyo.
Aliongeza “tunalazimika kulala
wawili wawili katika kitanda kimoja jambo ambalo linaweza kuhatarisha afya zetu
ukizingatia kuwa tumetoka katika familia tofauti tofauti na hatujuani afya
zetu” aliongeza.
Historia inaonyesha kuwa Chuo cha
ualimu Tarime kilianzishwa mwaka 1974 kama chuo cha ualimu daraja la III
C, mwaka 1981 serikali ilibadilisha programu na kuwa daraja la III B ili
kupata walimu wengi ambao waliitwa wa UPE (Universal Primary Education) huku
wengine wakiuita ualimu huo kuwa ni Ualimu Pasipo na Elimu.
Aidha mwaka 1990 ulianzishwa rasmi
mfumo wa Ualimu daraja la III A ambao unaendelea mpaka sasa kwa miundo
mbinu ile ile ya chuo iliendelea kutumiwa bila kufanyiwa ukarabati hadi hivi
sasa.
Hata hivyo wanachuo hao walisema
kuwa japo chuo hicho ni kati ya vyuo vikongwe vya ualimu hapa nchini kulingana
na historia yake, bado miundo mbinu yake ni mibovu na inahitaji kufanyiwa
ukarafati mkubwa ili kuendana na hadhi ya jina lenyewe.
“Huwezi amaini kuwa chuo hiki
ambacho kinatoa wataalamu na watu maarufu katika nchi hii ndio kinamwonekano
huu ambao hata wewe ukiingia ndani ya mabweni tunayolala utatuhurumia na
tunatoa fedha za ukarabati kwa kila mwaka shilingi 10,000/= kwa kila mwanchuo
ukipiga hesabu hizo fedha ni kiasi gani?”alihoji mwanachuo mwingine wa mwaka wa
pili.
Wanachuo hao walieleza kuwa
kero hiyo ni la miaka na mikaka ingawa kila wanapohoji huambiwa wao ni
chadema na kwa kuwa wameenda kutafuta mafunzo yenye ajira huamua kunyamaza huku
roho zikiendelea kuwauma kwa kukosa pa kusemea.
“Tunazibwa midomo hatuwezi kuongea
kwa madai kuwa anayeongea ni CHADEMA wakati hali halisi inayotukabili
inaonekana wazi. Na kutokana na hili inaonesha wazi kuwa chuo nacho
kimeingia kwenye siasa bila sisi kujuwa” alisema mwanachuo huyo wakati wa
mahojiano akiwa kwenye zoezi la utafiti wao wa kielimu kama sehemu ya
kukamilisha kazi yao ya mafunzo ya ualimu daraja la III A.
Mabweni ya wanachuo wa kiume hayana
madirisha hali inayokuwa tete zaidi ni wakati mvua inapoanza kunyesha hasa
yenye upepo maji hujaa ndani huku Godoro na shuka za wanachuo kulowana.
“Tunaomba serikali iangalie chuo
hiki ikipangie bajeti ya kukifanyia ukarabati ili wanachuo tufurahie kusomea
ualimu lakini sasa ukiingia bwenini tumeziba madirisha kwa maboksi !” Mmoja
wa wanachuo hao aliongea akionyesha masikitiko.
Mkuu wa chuo hicho Bw. Nicolaus
Magige alipotakiwa kuyazungumzia matitizo yanayokikabili chuo chake
alikana kuwepo kwa matatizo huku akikiri kuwepo kwa miundo mbinu
mibovu ya maji.
“Hatuna shida na siwezi kuilaumu
idara maji ya Wilaya ya Tarime kuwa chuo changu kinaupungufu wa maji ila miundo
mbinu ya maji ni ya zamani inahitaji ukarabati ili kufanya kazi
vizuri” alisema Bw. Magige kwa njia ya simu.
Na Waitara Meng'anyi-Tarime
Post a Comment