TAMKO LA NEC JUU YA KUPANDA KWA GHARAMA ZA MAISHA NCHINI.
Halmashauri Kuu ya CCM Taifa imejadili kwa kina suala la kupanda kwa
gharama za maisha nchini. NEC inakiri kwamba ni kweli lipo tatizo la
kupanda kwa gharama za maisha nchini. Tatizo hili pia limezikumba
karibu nchi nyingi za Afrika Mashariki na kwakweli karibu sasa lipo
dunia nzima. Baadhi ya sababu za kupanda kwa gharama za maisha hapa
nchini ni pamoja na;
1. Hali mbaya ya mavuno inayotokana na uhaba wa mvua au mvua kunyesha
kipindi cha nje ya msimu katika maeneo mengi nchini.
2. Kuongezeka kwa bei ya mafuta duniani, hivyo kuongezeka kwa gharama
za uzalishaji wa bidhaa na usafirishaji wa mazao.
3. Kuyumba kwa thamani ya dola ya Marekani.
4. Kuwepo kwa soko huria ambapo sasa mazao ya chakula yanapata soko
nje ya nchi, na wakati mwingine kuuzwa nje kwa njia ya magendo na
hivyo kusababisha uwepo wa ukubwa wa mahitaji na hivyo kuongezeka kwa
bei ya chakula nchini.
5. kuongezeka kwa walaji wakati uzalishaji ukiwa mdogo.
6. kutofanikiwa (ikiwemo kuhujumiwa na wafanyabiashara wasio
waaminifu) kwa baadhi ya mikakati ya kudhibiti mfumko wa bei.
Uwamuzi wa Halmashauri Kuu ya Taifa.
1. Pamoja na Serikali kuendelea kuchukua hatua za muda mrefu na wa
kati za kukabiliana na tatizo hili, CCM inaiagiza Serikali kuchukua
hatua za haraka za muda mfupi ikiwemo kuangalia upya baadhi ya kodi
katika vyakula pamoja na kodi ya ongezeko la thamani VAT katika
sukari.
2. Utaratibu wa ruzuku ya mbegu na mbolea upanuliwe ili kunufaisha
wakulima wengi.
3. Serikali iongeze kasi ya utekelezaji wa mpango wake wa kuongeza
uwezo wa kuhifadhi chakula nchini, hasa kwa kupitia Hifadhi ya Nafaka
ya Taifa, ikiwa ni pamoja na kujenga maghala zaidi ya mazao ya chakula
katika maeneo ya uzalishaji wa mazao, na kutenga fedha nyingi zaidi
kwa ununuzi wa mazao hayo. Pamoja na hili, mipango ifanywe kuongeza
uwezo wa wakulima kuhifadhi chakula chao wenyewe na kupunguza upotevu
baada ya mavuno (post-harvest losses).
3. Serikali iendelee kupanua utaratibu wake wa kutumia Hifadhi ya
Nafaka ya Taifa (SGR) kama nyenzo ya kudhibiti kupanda kwa bei za
vyakula. Wakati wa uhaba wa vyakula katika maeneo ya mijini, kasi ya
kupeleka chakula maeneo hayo iongezwe na utaratibu mzuri zaidi wa
usambazaji wa chakula utumike ili walaji, na sio wasafirishaji na
wasindikaji, wanufaike.
4. Serikali iongeze kasi ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya kilimo
nchini, hasa ASDP na SAGCOT, ambayo itasaidia kumaliza tatizo la
chakula nchini na kuongeza ajira na kipato kwa Watanzania walio
wengi.
5. Serikali idhibiti malipo ya huduma ya ndani kwa kutumia fedha za
kigeni, hasa dola za kimarekani. Aidha, Serikali iongeze udhibiti wa
Maduka na mahoteli yanayofanya biashara ya fedha za kigeni ili kuondoa
hujuma kwa uchumi wa nchi inayofanywa kutokana na uhuru uliokithiri
katika biashara hii.
6. Waajiri wahimizwe kupandisha mishahara na malipo mengineyo kwa
wafanyakazi wao ili waweze kumudu gharama za maisha.
7. Serikali iweke jitihada zaidi za kudhibiti ulanguzi wa bidhaa
muhimu na upandishaji holela wa bei za vyakula, kodi za nyumba na
usafiri.
Nape Moses Nnauye Chama Cha Mapinduzi
Ideology and Publicity Secretary
Post a Comment