MTANGAZAJI

ERTON C. KÖHLER KIONGOZI MKUU MPYA WA KANISA LA WAADVENTISTA ULIMWENGUNI

 


Katika jiji la St. Louis, Missouri, Marekani, Mkutano Mkuu wa 62 wa Konferensi Kuu ya Kanisa la Waadventista wa Sabato Ulimwenguni umemchagua Erton Köhler kuwa Kiongozi Mkuu wa Kanisa hilo Ulimwenguni  kwa kipindi cha miaka mitano.

Ni utaratibu wa kawaida kwa Kanisa la Waadventista wa Sabato Duniani kufanya mkutano wa Konferensi Kuu kila baada ya miaka mitano. Mkutano huu huwaleta pamoja wajumbe kutoka mataifa mbalimbali duniani kote, ambapo miongoni mwa shughuli zake kuu ni uchaguzi wa viongozi wa Kanisa kwa ngazi ya Konferensi Kuu yenye makao yake makuu Marekani, pamoja na viongozi wa Divisheni 13 duniani.

Kabla ya kuchaguliwa kwake, Erton Köhler alikuwa Katibu Mtendaji wa Kanisa la Waadventista wa Sabato Duniani nafasi aliyoianza rasmi Aprili 14, 2021. Kabla ya hapo, aliwahi kuwa Kiongozi wa Divisheni ya Amerika ya Kusini, akihudumu katika eneo hilo lenye nchi nane tangu mwaka 2007, alipochaguliwa akiwa na umri wa miaka 38 na kuwa mmoja wa viongozi vijana kwa jukumu hilo katika historia ya Divisheni hiyo.

Köhler alizaliwa kusini mwa Brazil mwaka 1969 asili yake ikiwa ni Ujerumani na tangu utotoni alitamani kufuata nyayo za baba yake ambaye alikuwa mchungaji wa Waadventista. Alipata Shahada ya Kwanza ya Theolojia mwaka 1989 katika Taasisi ya Mafunzo ya Waadventista, ambayo sasa ni Chuo Kikuu cha Waadventista cha Brazil. Mwaka 2008, alihitimu tena kutoka chuo hicho akiwa na Shahada ya Uzamili katika Theolojia ya Kichungaji. Kwa sasa, anaendelea na masomo ya Shahada ya Udaktari wa Huduma ya Kichungaji katika Chuo Kikuu cha Andrews nchini Marekani.

Kati ya mwaka 1990 hadi 1994, alikuwa mchungaji wa kanisa mahalia huko São Paulo. Baadaye, mwaka 1995, alichaguliwa kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Vijana wa Konferensi ya Rio Grande do Sul, kisha mwaka 1998 akawa Mkurugenzi wa Huduma za Vijana wa Unioni ya Kaskazini-Mashariki mwa Brazil. Mwaka 2002, alirejea katika Konferensi ya Rio Grande do Sul kama Katibu Mtendaji, na mwaka uliofuata akachaguliwa kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Vijana kwa nchi nane za Divisheni ya Amerika ya Kusini (SAD) kabla ya kuwa Kiongozi wa Divisheni hiyo mwaka 2007.

Köhler amemuoa Adriene Marques, ambaye ni muuguzi, na wamejaliwa watoto wawili. Pamoja, wamekuwa mstari wa mbele katika huduma ya kanisa, wakihudumu bega kwa bega na kutembelea waumini duniani kote. Amekuwa akisisitiza mitazamo thabiti kuhusu athari za michezo ya kompyuta kwa vijana, upendeleo wa muziki unaojenga imani, na umuhimu wa kushikilia imani kuliko kuhusika kisiasa.

Katika nafasi yake mpya, Köhler ataongoza Kanisa la Waadventista wa Sabato Duniani akiwa ni kiongozi mkuu wa kiutawala. Atasaidia kuunda maono ya kimkakati ya utume wa  Kanisa hilo lililoko katika nchi zaidi ya 200 duniani, kutoa mwongozo wa mafundisho, na kuunganisha maeneo mbalimbali kupitia utume wa pamoja. Atakuwa mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Utendaji ya Konferensi Kuu, mabaraza kadhaa ya kanisa, na atashirikiana kwa karibu na viongozi wa Divisheni, akiwakilisha kanisa katika matukio makubwa ya kimataifa.

Pia anatarajiwa kuhamasisha mipango ya utume wa dunia, kuhakikisha uthabiti wa mafundisho ya Waadventista, na kuimarisha taasisi za elimu, afya, na vyombo vya habari vya kanisa hilo.

Kanisa la Waadventista wa Sabato limekuwa dhehebu la Kiprotestanti la kimataifa tangu mwaka 1863, likiwa na zaidi ya waumini milioni 23 kote duniani. Biblia inatambuliwa kuwa mamlaka kuu ya mafundisho ya kanisa, na ujumbe wake ni kuwasaidia watu kupata uhuru, uponyaji, na tumaini katika Yesu Kristo.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.