MTANGAZAJI

WAZIRI MKUU PINDA AONYA KUHUSU KUCHEZEA AMANI TANZANIA

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewaonya wakazi wa Manispaa ya Bukoba na Watanzania wote kwa ujumla kuacha kuchezea hali ya amani ambayo imekuwepo kwa muda mrefu hapa nchini.

Ametoa onyo hilo jana jioni (Ijumaa, Machi 4, 2011), wakati akijibu risala ya Wazee wa Manispaa hiyo ambao waliwaomba Watanzania wote waitunze amani na wasikubali kudanganywa na kauli za uchochezi zenyelengo la kuwatia hofu na kuwakatisha tamaa.

Akizungumza na maelfu ya wakazi wa Manispaa ya Bukoba kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Mayunga (Uhuru Platform),Waziri Mkuu alisema: “Wana-Kagera mnajua maana ya vita kwa sababummepata rasharasha mwaka 1972 wakati Idd Amin aliposema anataka aje kunywa chai Mwanza lakini ninyi pia ni mashahidi wa vita halisi ya mwaka 1978,” alisema.


“Hivi majuzi tumepata matatizo kule Gongo la Mboto, wakati watu wanakimbia kuokoa maisha yao, wako wengine waaliokuwa wakikimbilia  kwenye nyumba za wenzao ili kuiba mali zilizoachwa. Ni ajabu iliyo kumsikia mtu akitamka: Bora vurugu bwana!” alishangaa.


  Alisema kama kamwe wananchi wasikubali uchochezi huo kwani maandamano na vurugu siyo suluhisho na amani ikishapotea kuirudisha ni gharama kubwa mno.

“Kila kukicha, kuna watu wanazua madai ya kila aina, mara kura zimeibiwa, mara Katiba mpya; walichoamua ni kutembea nchi nzima …pengine hawana kazi za kufanya ndiyo maana wanatembea kuitisha
maandamano huku na kule,” alisema.

Alisema: “Kama suala ni kuing’oa CCM madarakani ni laima wajiulize maswali ya msingi ni vipi wataweza kuindoa CCM katika matawi, mashina, kwenye kata na tena mjijengee uhalali kwa wananchi hadi wawakubali.”


“Msipofanya hivyo, mtatembea weee lakini CCM haingoki ngo!,” alionya na kuongeza kwamba: “Uongozi unategemea wananchi wanavyotutazama… wanatupima, je watu hawa wataweza kutusaidia? Je watajali shida zetu?”alitahadharisha.

Mapema, katika risala yao iliyosomwa na Mzee Haruna Almasi, wazee hao waliomba kupatiwa matibabu bila mlolongo mrefu ili wasihangaike.“Tunaomba Serikali ituwekee utaratibu mwepesi wa kuwasaidia wazee

  kupata tiba…”, alisema Mzee Almasi.


Wazee hao ambao walisema wanaiunga mkono hotuba ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa Februari 28, 2011 wakati akilihutubia Taifa, pia waliomba kuwe na uwakilishi wa wazee katika ngazi mbalimbali za vikao vya
  kufanya maamuzi kuanzia kwenye Serikali za Mitaa hadi Bungeni.


Leo(Jumapili, Machi 6, 2011), Waziri Mkuu atakuwa wilayani Chato ambako anatarajiwa kuweka jiwe la msingi katika jengo la Halmashauri a Wilaya hiyo na kufungua SACCOS ya Mshikamano kabla ya kuzungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara kwenye shule ya msingi ya Chato.


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
 JUMAMOSI, MACHI 05, 2011

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.