MTANGAZAJI

WATAALAMU WAONYA KUHUSU AI NA IMANI ZA WATU

Viongozi wa dini, wanazuoni, wanasheria na watetezi wa haki za binadamu kutoka madhehebu mbalimbali wamekutana katika  Chuo cha Newbold  nchini Uingereza kujadili athari za teknolojia ya Akili Unde (AI) kwa uhuru wa dini, dhamiri ya mtu binafsi na haki za msingi za binadamu. Mkutano huo uliandaliwa na Chama cha Kimataifa cha Uhuru wa Dini (IRLA) chini ya kaulimbiu ya "Uhuru wa Dini katika Enzi ya Teknolojia Zinazoibuka."

Washiriki walitoka katika makundi mbalimbali ya kidini ikiwemo Waadventista wa Sabato, Wakatoliki, Waprotestanti, Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho (LDS), Waislamu pamoja na watu wasiofungamana na dini yoyote.

Miongoni mwa watoa mada walikuwa ni Nicholas P. Miller wa Chuo cha Kikuu cha Waadventista cha Washington nchini Marekani, James Standish aliyewahi kuhudumu katika Tume ya Marekani ya Uhuru wa Dini Kimataifa, W. Cole Durham Jr. wa Chuo Kikuu cha Brigham, Andreea Beatrice Popa jaji nchini Romania, Alyssa Truman kutoka Makao Makuu ya Kanisa la Waadventista Ulimwenguni, na Gifford Rhamie wa Newbold College.

Washiriki walionya kuwa mifumo ya Akili Unde ina uwezo wa kushawishi namna watu wanavyofikiri, kuamini na kufanya maamuzi kupitia algoriti zinazochagua taarifa wanazoona mtandaoni. Walisema hali hiyo inaweza kuhatarisha uhuru wa dhamiri na uhuru wa mawazo ambao kwa muda mrefu umehifadhiwa kama haki ya msingi ya binadamu.

Mkutano huo pia ulijadili masuala ya ufuatiliaji wa kidijitali, faragha ya taarifa za kidini, ubaguzi unaoweza kusababishwa na matumizi ya data, pamoja na matumizi ya chatbots za kidini zinazoweza kuonekana kama viongozi wa kiroho kwa watumiaji. 

Viongozi wa dini walitoa wito kwa taasisi za kidini kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya teknolojia mpya ili kuhakikisha kwamba mifumo ya AI inaheshimu imani mbalimbali na kulinda uhuru wa kufikiri, kuamini na kuabudu.

Katika mjadala mwingine, viongozi wa Kanisa la Waadventista walikiri umuhimu wa kuendelea kukuza mazingira ya mazungumzo ya wazi, kuheshimu mitazamo tofauti na kulinda uhuru wa dhamiri ndani ya taasisi za kidini. 

Kwa mujibu wa washiriki, maendeleo ya AI yanaleta fursa nyingi kwa jamii, lakini yanahitaji kusimamiwa kwa umakini ili kulinda utu wa mwanadamu, uhuru wa dini na haki za msingi za binadamu.



No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.