MTANGAZAJI

SAD YAPITISHA SERA MPYA KWA WACHUNGAJI WAADVENTISTA



Divisheni ya Amerika Kusini ya Kanisa la Waadventista wa Sabato (SAD)  imeidhinisha mabadiliko katika sera zake za kiutawala yanayolenga kupunguza uhamisho wa mara kwa mara wa wachungaji na kuimarisha utendaji wa huduma ya kichungaji. Hatua hiyo ilipitishwa na wajumbe wa Baraza la Mwaka la divisheni hiyo lililofanyika hivi karibuni. 

Kwa mujibu wa kanuni hizo mpya zilizochapishwa katika tovuti rasmi ya SAD, eneo la kiutawala linlojumuisha nchi za Bolivia, Brazil, Chile, Ecuador, Paraguay, Peru, Uruguay na Argentina, imepitisha sera mpya zinazolenga kupunguza uhamisho wa wachungaji na kuimarisha utendaji wa huduma ya kichungaji na utekelezaji wa kuwaweka wakfu wachungaji husika. 

Kuwekwa wakfu (kuwekewa mikono) ni hatua ya juu kwa wachungaji wa kanisa la Waadventista wa Sabato Duniani ambapo huwaongezea majukumu ya kiutendaji ya kiroho ikiwemo kubatiza, kufungisha ndoa na wanaweza kutekeleza majumu yao mahali popote duniani wanapotakiwa kufanya hivyo. 

Sera hiyo  inawataka wanaoandaliwa kwa huduma ya kuwekwa wakfu kuhudumu ndani ya taasisi au eneo moja ama mawili tu. Pia hawataruhusiwa kuhudumu katika ngazi ya  ukurugenzi wa idara au uongozi wa taasisi katika kipindi cha mchakato wa kuwekwa wakfu.

Baada ya kuhitimu masomo ya uchungaji  na kupokea rasmi mwito wa huduma ya kichungaji, kipindi cha maandalizi kitadumu kwa angalau miaka minne na si zaidi ya miaka sita, huku tathmini ikifanyika kila mwaka. Wanaopata tathmini mbili zisizoridhisha au wanaofikisha mwaka wa sita bila kuwekwa wakfu hawataruhusiwa kuendelea na huduma ya kichungaji. Kwa wale ambao hawajafunga ndoa, muda wa juu wa kuhudumu kabla ya kuwekwa wakfu ni miaka kumi na miwili.

Kwa wachungaji waliowekwa wakfu, sera mpya inaweka kiwango cha chini cha miaka minne ya kuhudumu katika eneo moja, ambapo muda huo unaweza kuongezwa hadi miaka mitano au zaidi kulingana na mazingira na mahitaji yaliyopo. 

Sera hiyo pia inaonesha kuwa viongozi  na wakurugenzi wa idara wanapaswa kubaki katika nafasi zao kwa kipindi chote cha muhula wa utawala, wakiepuka uhamisho au mabadiliko ya majukumu. Isipokuwa kuwe sababu za msingi za kutosha na baada ya mashauriano ya awali na viongozi wa ngazi za juu.

 Azimio hilo linasisitiza kuwa ni njia ya kuimarisha malezi ya kichungaji, mipango ya huduma za kanisa, na kusaidia ustawi wa familia za watumishi wa kanisa ikiwemo wachungaji.

Kwa mujibu wa takwimu za Adventist Archieve za mwaka 2025,  Divisheni ya Amerika Kusini ya Kanisa la Waadventista wa Sabato ina waumini zaidi ya milioni 2.7,  wachungaji wenye leseni wapatao 1,323 na waliowekwa wakfu 4,045  wanaohudumu katika eneo hilo.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.