RAIA WA KENYA WATUHUMIWA ULAGHAI WA FEDHA ZA ELIMU MAREKANI
Mamlaka nchini Marekani zimetagaza kuwafungulia mashtaka watu watano wanaotuhumiwa kuhusika katika mtandao wa ulaghai wa misaada ya elimu unaodaiwa kuhusisha baadhi ya raia wa Kenya.
Hatua hiyo ni sehemu ya operesheni maalum iliyopewa jina la Ghostbusters, inayolenga kudhibiti wizi wa fedha za wanafunzi kupitia mifumo ya misaada ya fedha za serikali.
Kwa mujibu wa Wizara ya Haki ya Marekani, watuhumiwa wanadaiwa kutumia vitambulisho vya raia wa Marekani vilivyoibwa kuunda maombi ya uongo ya misaada ya fedha za serikali kwa wanafunzi, maarufu FAFSA, na kisha kuwaandikisha wanafunzi hewa katika vyuo mbalimbali ili kupata fedha za hizo kinyume cha sheria.
Maafisa wa uchunguzi wanasema baada ya fedha hizo kutolewa, zilielekezwa kwenye akaunti zilizokuwa chini ya udhibiti wa mtandao huo badala ya wanafunzi halali. Serikali ya Marekani imeeleza kuwa zaidi ya dola 750,000 za Marekani katika mfumo wa sarafu za kidijitali zimekamatwa zikihusishwa na wahusika wa mtandao huo.
Miongoni mwa waliotajwa katika nyaraka za mashtaka ni Francis Mogambi, raia wa Kenya anayekabiliwa na tuhuma za kutumia taarifa za watu wengine kupata misaada ya wanafunzi kwa njia ya udanganyifu.
Akizungumza wakati wa kutangaza maendeleo ya uchunguzi huo, Colin M. McDonald wa Kitengo cha Kitaifa cha Uhalifu wa Udanganyifu nchini Marekani alisema mamlaka zitaendelea kuwafuatilia watuhumiwa bila kujali walipo, ikiwemo nchini Kenya.
Uchunguzi wa sakata hilo bado unaendelea huku mamlaka zikiahidi kuchukua hatua zaidi dhidi ya wote watakaobainika kuhusika na mtandao huo wa ulaghai wa fedha za serikali kwa ajili ya wanafunzi.

.png)
Post a Comment