MTANGAZAJI

SERA ZA UHAMIAJI MAREKANI ZINAVYOATHIRI MAKANISA YA WAADVENTISTA KUTOKA AFRIKA.

 


Waumini wa Kanisa la Waadventista wa Sabato wenye asili ya Afrika ni miongoni mwa makundi yanayoathiriwa na mabadiliko ya sera za uhamiaji nchini Marekani, huku viongozi wa dini wakionya kuwa hofu ya kukamatwa na mamlaka za uhamiaji imeanza kupunguza ushiriki wa baadhi ya waumini katika shughuli za ibada na kijamii. Takwimu za kituo cha utafiti cha Pew zinaonyesha kuwa hadi Juni 2025, Marekani ilikuwa na wahamiaji milioni 51.9, sawa na asilimia 15 ya wakazi wote wa nchi hiyo.
 
Kanisa la Waadventista nchini Marekani lina makanisa ya waumini kutoka mataifa ya Afrika, ikiwemo Kenya, Tanzania, Uganda, Nigeria, Ghana, Ethiopia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Ingawa hakuna takwimu rasmi zinazoonyesha idadi ya Waadventista Waafrika walioathiriwa moja kwa moja, ripoti kutoka makanisa ya wahamiaji nchini humo zinaonyesha kuwa kuondolewa kwa ulinzi wa maeneo nyeti kama nyumba za ibada kumeongeza hofu miongoni mwa waumini wahamiaji.
 
Kwa mujibu wa Religion News Service na ripoti za makanisa ya wahamiaji, baadhi ya makanisa yenye waumini wengi wahamiaji yameripoti kushuka kwa mahudhurio kwa takribani asilimia 20 kutokana na hofu ya operesheni za uhamiaji. Katika baadhi ya maeneo, mahudhurio yalishuka kutoka wastani wa watu 2,500 hadi chini ya 2,000 katika vipindi vya ibada vya mwishoni mwa juma.
 
Wachambuzi wa masuala ya dini wanasema hali hiyo inaweza kuathiri pia makanisa ya Waadventista yenye waumini kutoka Afrika, kwa kuwa sehemu kubwa ya ukuaji wa baadhi ya makanisa  ya Waadventista nchini Marekani inatokana na jamii za wahamiaji. Aidha, takwimu za Pew zinaonyesha kuwa wahamiaji wanachangia asilimia 19 ya nguvu kazi ya Marekani, jambo linaloonyesha mchango wao mkubwa katika uchumi na maisha ya kijamii ya taifa hilo.
 
Viongozi wa kidini wameendelea kutoa wito wa kulindwa kwa uhuru wa kuabudu na kuhakikisha kuwa makanisa yanaendelea kuwa maeneo salama kwa waumini wote bila kujali asili yao ya kitaifa au hali yao ya uhamiaji.
 

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.