HITILAFU YA MAWASILIANO YAKWAMISHA SAFARI ZA NDEGE MAREKANI
Marekani imekumbwa na moja ya msukosuko mkubwa katika sekta ya usafiri wa anga baada ya hitilafu ya mawasiliano kuathiri vituo vya kudhibiti safari za ndege na kulazimisha Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya nchi hiyo (FAA) kusimamisha kwa muda safari zote za ndege zinazotarajiwa kuondoka katika viwanja vya ndege nchini kote Novemba 13, mwaka huu.
Hatua hiyo ya dharura ilichukuliwa kwa sababu za usalama baada ya mifumo ya mawasiliano katika vituo vya usimamizi wa safari za anga kushindwa kufanya kazi kawaida.
Taarifa zinaeleza kuwa tatizo hilo liliathiri vituo 22 vya kudhibiti safari za anga vinavyoongoza ndege zinazopita katika anga ya Marekani, hali iliyosababisha mamia ya ndege kuzuiwa kuondoka na nyingine kubadilishwa njia.
Athari za tukio hilo zimekuwa kubwa kwa wasafiri na mashirika ya ndege. Kwa mujibu wa kampuni ya ufuatiliaji wa safari za ndege ya FlightRadar24, zaidi ya safari za ndege 4,700 zilifutwa huku zaidi ya safari 10,000 zikicheleweshwa katika siku moja pekee. Aidha, zaidi ya safari 700 za siku inayofuata zilikuwa tayari zimefutwa kutokana na athari zinazoendelea za hitilafu hiyo.
Wataalamu wa usafiri wa anga wanasema huenda ikachukua siku kadhaa kwa mashirika ya ndege kurejesha ratiba zake za kawaida kutokana na msongamano wa abiria, ndege na wafanyakazi uliojitokeza baada ya kusimamishwa kwa safari hizo.
Tukio hilo limeelezwa kuwa la kwanza kwa kusimamishwa kwa safari zote za ndege nchini Marekani tangu mwaka 2023 na la pili kwa ukubwa tangu mashambulizi ya Septemba 11 mwaka 2001.
Maafisa wa usalama wa taifa la Marekani wamesema hadi sasa hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa tukio hilo limesababishwa na shambulio la kimtandao. Badala yake, uchunguzi wa awali unaelekeza kwenye hitilafu ya mawasiliano na vifaa vya mfumo wa usimamizi wa usafiri wa anga.
Ingawa FAA imeanza kuruhusu baadhi ya safari kuendelea, maelfu ya abiria bado waliendelea kukabiliwa na ucheleweshaji wa safari, kubadilishwa kwa ratiba na usumbufu mkubwa katika viwanja vya ndege mbalimbali nchini Marekani.

.png)
Post a Comment