MTANGAZAJI

WAHAMIAJI WA AFRIKA MASHARIKI UGHAIBUNI

 


Katika ulimwengu wa leo, maelfu ya vijana na wazee kutoka Kenya, Uganda, Tanzania, Ethiopia, Somalia na nchi zingine za Afrika Mashariki wameamua kuhamia nchi za ng’ambo na wengine bado wanafanya jitihada hizo ili kutafuta maisha bora. Lengo likiwa ni kuboresha maisha yao na kusaidia familia zao zinazowategemea nyumbani

Hata hivyo, safari hii si rahisi, kwani kuna vikwazo kazaa vinavyowakabili huku wakijitahidi kutuma pesa ambazo zimekuwa nguzo muhimu ya uchumi wa maeneo wanakotoka.

Mchango Mkubwa wa Diaspora

Utumaji wa pesa  zimekuwa “mafuta” ya uchumi wa Afrika Mashariki. Kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Dunia na vyanzo vingine vya hivi karibuni vinaonyesha kuwa Kenya ilipokea karibu dola za kimarekani bilioni 4.8 hadi 5.1  mwaka 2024, ikionyesha ongezeko la 14-18% kutoka mwaka uliopita. Baadhi ya ripoti zinaonyesha  zaidi ya bilioni 7  katika kipindi cha miezi 12. Marekani inachangia zaidi ya 40% ya pesa hizi.

Uganda ilipokea zaidi ya dola bilioni 1.2, wakati Ethiopia na nchi zingine zilipokea mamia ya mamilioni. Jumla ya pesa zilizotumwa  kwa eneo la Afrika Mashariki ilizidi  dola bilioni 5 katika miaka ya karibuni, na katika eneo la Afrika Kusini mwa Sahara ikifikia karibu dola za kimarekani bilioni 49-95.

Pesa hizi hutumika kwa mahitaji ya kila siku ikiwemo chakula, elimu ya watoto, matibabu, na hata kuanzisha biashara ndogo nyumbani. Katika baadhi ya familia, pesa hizi ndio chanzo pekee cha mapato.
 

 Baadhi ya Matatizo wanayokabiliana nayo wanaafrika mashariki walikooko ughaibuni yako ya aina tofautitofauti huku yakihitaji  bidii na subira. Miongoni mwa matatizo hayo ni 
1. Shinikizo la Kazi na Uchumi 

Wengi hufanya kazi za chini ikiwemo  wafanyakazi wa hospitali, usalama, ujenzi au huduma za nyumbani hata wakiwa na vyeti vya elimu ya juu. Hii inasababisha upotevu wa rasilimali watu wenye ujuzi na kupunguza mapato yao binafsi ili waweze kutuma pesa nyumbani.

2. Ubaguzi na Matatizo ya Ujumuishaji 
Ubaguzi wa rangi na kiuchumi bado ni tatizo kubwa katika baadhi ya nchi ikiwemo Marekani, Uingereza na zinginezo barani Ulaya. Wanapata shida kupata nyumba, kazi bora au hata huduma za msingi. Katika nchi za Ghuba, baadhi hukabiliwa na unyanyasaji wa wafanyakazi.

3. Afya ya Akili  
Shinikizo la kutuma pesa nyumbani kila mwezi, kujitenga na familia, na changamoto za kila siku husababisha wasiwasi, unyogovu na hata msongo wa mawazo. Wengi hupuuza matatizo haya kutokana na aibu au ukosefu wa huduma zinazofaa kiutamaduni.

4. Gharama za Maisha na Uhamiaji  
Gharama za kuishi ikiwemo kodi, chakula, usafiri ni kubwa, na gharama za kutuma pesa bado ni juu wastani wa 6-8%. Hii inawafanya wahamiaji kupunguza matumizi yao wenyewe ili familia zao ziweze kujikimu.


Licha ya matatizo haya, wahamiaji wa Afrika Mashariki wameonyesha ustahimilivu mkubwa kwani wanafanya kazi mbili au tatu ili kuongeza mapato, hushirikiana kupitia vikundi vya jamii, makanisa na mitandao ya kijamii. Pesa wanazotuma huboresha maisha ya familia na kuchangia miradi ya maendeleo nyumbani. 


Wahamiaji wa Afrika Mashariki wanaandika hadithi ya ushujaa kila siku, wanapambana na maisha magumu ughaibuni ili kuhakikisha familia zao zinajikimu na kuendelea mbele.  Serikali, mashirika na jamii zinapaswa kuwapa msaada zaidi ili kupunguza gharama za kutuma pesa kutoa huduma bora za afya ya akili, na kuwalinda dhidi ya ubaguzi.

Chanzo: Takwimu kutoka Benki ya Dunia, IOM, Benki Kuu ya Kenya 2023-2025.



No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.