MTANGAZAJI

MAKANISA YA KIPROTESTANTI MAREKANI YALIPUNGUA MWAKA 2024.



Idadi ya makanisa ya Kiprotestanti nchini Marekani imeendelea kupungua kwa mwaka 2024, baada ya makanisa yaliyofungwa kuzidi yale mapya yaliyoanzishwa, kwa mujibu wa utafiti wa kituo cha utafiti cha Lifeway.

Takwimu zinaonesha kuwa takribani makanisa mapya 3,800 yalianzishwa mwaka jana, huku karibu makanisa 4,000 yakifungwa, hali iliyopelekea upungufu wa jumla wa takribani makanisa 200 kote nchini.

Utafiti huo, uliotegemea taarifa kutoka madhehebu 35 ya Kikristo, unaonesha kuwa mabadiliko hayo yanatokana na kupungua kwa idadi ya watu wanaojitambulisha kama Wakristo pamoja na kushuka kwa mahudhurio ya ibada.

Hata hivyo, watafiti wanasema pengo kati ya kufunguliwa na kufungwa kwa makanisa limepungua ikilinganishwa na miaka ya nyuma. Kwa mfano, mwaka 2019 Marekani ilipoteza takribani makanisa 1,500.

Mkurugenzi Mtendaji wa Lifeway Research, Scott McConnell, amesema makanisa mengi bado yanaendelea kuwepo licha ya changamoto, ingawa mengi ni madogo na yana rasilimali chache.

Utafiti huo pia umebaini kuwa uanzishwaji wa makanisa mapya unaendelea kuwa muhimu, hasa katika jamii mpya, kwani makanisa yaliyoanzishwa hivi karibuni yanaonesha ukuaji mkubwa kuliko yale ya zamani.

Licha ya hali hiyo, asilimia 94 ya wachungaji wa Kiprotestanti wanasema wana imani makanisa yao yataendelea kuwepo katika kipindi cha miaka kumi ijayo, ingawa wasiwasi unaonekana zaidi katika makanisa yenye waumini wachache.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.