MIVUTANO YACHELEWESHA SHERIA YA AMRI KUMI TEXAS
Gavana wa jimbo la Texas,Marekani Greg Abbott, ameendelea na juhudi zake za kuhakikisha kwamba Amri Kumi zinasomwa katika shule za msingi na sekondari kote jimboni humo.
Hatua hii inakuja ikiwa ni sehemu ya mpango wa kudumisha maadili na misingi ya kidini miongoni mwa vijana, na pia kuimarisha "heshima kwa sheria na maadili ya familia" katika jamii.
Gavana Abbott alisema hivi karibuni, kuwa Amri Kumi ni muhimu katika kuimarisha maadili ya vijana na kuwatayarisha kwa maisha bora ya kijamii. Alisisitiza kuwa sheria hii itachangia kuboresha utamaduni wa heshima na utawala wa sheria katika jamii ya Texas.
Hata hivyo, hatua hii imekuwa kivutio cha mivutano ya kisheria na kijamii, huku wakosoaji wakidai kuwa utekelezaji wa amri hiyo unakiuka haki za kiraia na uhuru wa dini.
Kwa upande mwingine, Gavana Abbott anasisitiza kuwa ni jukumu la serikali kuhimiza maadili ya dini katika shule za umma, licha ya upinzani unaotoka kwa baadhi ya makundi ya haki za binadamu.
Majimbo mengine ambayo yameitekeleza sheria hii ni pamoja na Oklahoma ambako Gavana Kevin Stitt alitia saini sheria inayotaka amri kumi kusomwa katika shule za umma, jimbo la Florida sheria ya Amri Kumi kusomwa katika shule za msingi na sekondari ilipitishwa na kutekelezwa mwezi Aprili mwaka huu,Mississippi sheria hiyo pia ilipitishwa, ikiwa na lengo la kuimarisha maadili ya kidini katika elimu na Tennessee walianzisha mchakato wa kuhakikisha amri kumi zinajumuishwa kwenye mtaala wa elimu ya umma katika shule za sekondari.
Vita vya kisheria vimeendelea, na baadhi ya shule za wilaya tayari zimechukua msimamo tofauti, zikisema kuwa utekelezaji wa sheria hii unaweza kuvunja misingi ya katiba ya Marekani, hasa kuhusu kutenganisha dini na serikali.
Mahakama ya Shirikisho ilizuia utekelezaji wa amri hiyo katika baadhi ya maeneo, huku kesi hii ikiendelea kusikilizwa katika taasisi za kisheria.
Makundi ya haki za kiraia, pamoja na wazazi na walimu, wanashinikiza kwamba Amri Kumi hazipaswi kuingizwa katika muktadha wa elimu ya umma, kwani inaweza kuathiri uhuru wa mawazo na haki za wanafunzi.
Suala hili linazidi kuwa la muktadha wa kitaifa, na inasubiriwa kwa hamu kuona ni jinsi gani Mahakama Kuu ya Marekani itavyoshughulikia changamoto hii inayohusiana na dini, elimu na haki za kiraia.
Post a Comment