MTANGAZAJI

MAFUNZO ANWANI ZA MAKAZI NA POSTIKODI

  
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari nchini Tanzania Dkt. Jim Yonazi amefunga mafunzo ya utekelezaji wa anwani za makazi na postikodi kwa njia ya mkutano mtandao kwa wataalam wa Tanzania Bara na Zanzibar yaliyofanyika kwenye vituo vinne vya mkoa wa Mwanza, Mbeya, Tanga na Zanzibar.

Dkt. Yonazi amewataka wataalam hao 422 waliopatiwa mafunzo hayo ambapo wataalam 389 wametoka Tanzania Bara na 33 wametoka Zanzibar kwenda kutekeleza mafunzo hayo kwa vitendo kwa kuweka namba za nyumba, majina ya mitaa na barabara kwenye halmashauri wanazotoka ili kuhakikisha kuwa anwani za makazi zinatekelezwa nchi nzima na kukamilika ifikapo mwezi Mei mwaka huu.

Ameongeza kuwa utekelezaji wa anwani za makazi na postikodi utasaidia kufungua kasi ya uchumi, utoaji wa huduma za kijamii kwa wananchi na kuifungua Tanzania kidijitali, “mwananchi yeyote atatambulika duniani na anaweza kufikiwa na mteja kwa ajili ya kuuza bidhaa au huduma, hivyo kila mwananchi awiwe kuwa na namba ya nyumba, jina la barabara au mtaa anapoishi,” amesema Dkt. Yonazi.

Pia, ametoa wito kwa kampuni, wadau mbali mbali na familia kuchangia utekelezaji wa anwani za makazi na postikodi na kila mmoja awe balozi wa anwani za makazi na wataalam watoe taarifa kwa viongozi wao na Wizara iko tayari kuendelea kushirikiana kutekeleza hili.

Naye Mratibu wa Kitaifa wa Anwani za Makazi na Postikodi wa Wizara hiyo, Mhandisi Jampyion Mbugi, amesema kuwa wataalam waliopatiwa mafunzo hayo ni wataalam wawili kutoka kwenye kila halmashauri nchini Tanzania ambapo inahusisha wataalam wa TEHAMA, Ardhi, Mipango Miji na Ramani ambapo wamepatiwa mafunzo hayo kwa muda wa juma  moja kuanzia Januari  17  mwaka huu ya utekelezaji wa anwani za makazi na postikodi ikiwemo kuweka namba za nyumba, jina la mtaa au barabara na kuweka taarifa za maeneo hayo kwenye mfumo wa kielektroniki wa NAPA ili anwani hizo zipatikane na kutumiwa na wananchi kwa kuwawezesha kutoka eneo moja kwenda eneo lingine kwa kutumia simu ya mkononi au kompyuta.

Akitoa salamu za shukrani kwa niaba ya wataalam wengine waliopatiwa mafunzo hayo, Afisa Mipango Miji wa Halmashauri ya Kilindi, Tanga ndugu Anastius Biswalo Manumbu amesema kuwa wamepatiwa mafunzo hayo kwa vitendo na wataenda kuwafundisha wataalam wengine ili kuhakikisha kuwa anwani za makazi zinakamilika kwa wakati kuendana na azma ya Serikali na watazingatia miongozo iliyopo ya uwekaji wa anwani za makazi na postikodi.


No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.