MTANGAZAJI

WAKUU WA MIKOA WATAKIWA KUSIMAMIA UTEKELEZAJI WA ANWANI ZA MAKAZI TANZANIA

 

 
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari nchini Tanzania Nape Nnauye amewataka wakuu wa mikoa nchini kusimamia vyema zoezi la utekelezaji wa uwekaji wa anwani ya makazi ili liweze kukamilika katika muda uliopangwa.

Akizungumza katika ufunguzi ma mafunzo ya utekelezaji wa mfumo huo  ambayo yalifanyika kwa njia ya Mkutano Mtandao(Video conference) Jijini Dar es Salaam, yakihusisha Halmashauri 163 za Tanzania Bara na Mikoa 12 ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiwemo ushiriki wa Wakuu wa Mikoa hiyo nawataalam wao, Waziri Nape amesema kuwa utekelezaji wa jambo hilo ni muhimu kwani Sekta ya Mawasiliano ni wezeshi kwa sekta nyingine nchini.

“Mawasiliano ni Sekta muhimu na mtambuka kwani sekta zote zinategemea mawasiliano ili ziweze kufanya kazi kwa ufanisi, zoezi la utekelezaji wa anwani za makazi ni jambo ambalo litawasaidia wananchi kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa katika kujiletea maendeleo”, amesema Waziri Nape.

Waziri Nape alisema kuwa utekelezaji ni jambo muhimu ambapo Tanzania inatekeleza mfumo huo kwa kuzingatia Sera ya Taifa ya Posta ya Mwaka 2003,  pamoja na miongozo ya Umoja wa Posta Afrika na Umoja wa Posta Duniani ambapo Tanzania ni nchi mwanachama.

Utekelezaji wa mfumo huo ni moja kati ya mikakati ya kuiweka nchi katika mfumo wa kidijitali ili kurahishisha upatikanani wa huduma kwa wananchi pamoja na kurahisisha biashara ya mtandaoni.
 
Aidha, Waziri Nape alisema kuwa utekelezaji wa Anwani za makazi itakuwa ni zoezi ambalo litarahisisha zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 ambayo itafanyika Agosti mwaka huu na itakuwa rahisi kwa sababu ya upatikanaji wa anwani za makazi.

Katika hatua nyingine mafunzo hayo yalifunguliwa kwa mkoa wa Dar es Salaam ambapo Waziri Nape aliwataka viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwaelimisha wananchi kwani ndiyo wanaviongozi wengi katika mitaa mbalimbali nchini.

Waziri Nape alieleza jinsi mkoa wa Dar es Salaam unahitaji utekelezaji wa haraka wa utambuzi na uwekaji wa anwani za mitaa pamoja na nyumba ambapo kata 46 kati ya 102 ndizo zoezi hilo limetekezwa lakini kwa ujumla majina 85,728 ya barabara yanahitajika na vibao milioni moja vya nyumba vinahitajika ili kazi hiyo ikamilike.

Akizungumza, awali katika ufunguzi wa mafunzo hayo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Jim Yonazi, amesema kuwa mfumo wa anwani ya makazi ni muhimu sana kwa wananchi.

“Mfumo wa anwani za makazi ni muhimu sana katika kutambua makazi, sehemu za huduma za jamii na sehemu za biashara kwa hiyo tunalo jukumu na wajibu mkubwa ili zoezi na mfumo huu liweze kukamilika kwa wakati”, alisema Dkt. Jim Yonazi.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Amour Bakari, amesema kuwa kwa upande wao zoezi lilianza katika meneo manne ambapo utekelezaji wake unaendelea vizuri.

“Zoezi hili tumelianza na linaendelea vizuri, Wizara inashirikiana vizuri na Serikali za Wilaya kuhakikisha kuwa zoezi na utekelezaji wa mfumo huu unafanyika kwa ufanisi mkubwa ili kuwawezesha wananchi kufanya kazi na kujiletea maendeleo”, Alisema Amour.

Katika hatua nyingine, Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Macrice Mbodo alieleza jinsi mfumo huu wa anwani za makazi utakavyorahisisha biashara mtandao ambapo kwa sasa Shirika la Posta lina Jumla ya maduka 600 kupitia duka lake Mtandao (Posta Online Shop) ambayo kwa uhakika yanategemea upatikanaji wa anwani za makazi katika maeneo mbalimbali nchini na nje ya nchi.

Mbodo aliongeza kuwa zoezi la utekelezaji wa mradi wa Anwani ya Makazi na Posta likikamilika kwa nchi nzima litawapa wananchi nafasi ya kufanya kazi na kujipatia muda mwingi kufanya kazi za maendeleo kwani Posta itawahudumia kwenye masuala ya ununuzi wa bidhaa kupitia duka mlangoni.
 
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amosi Makala amesema kuwa wako tayari kutekeleza mradi huo kwani umekuja muda mwafaka kwani Mkoa wa Dar es Salaam uko katika utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mipango Miji ambao unalenga kuliboresha Jiji la Dar es Salaam.

“Jambo hili limekuja muda mwafaka kabisa kwani kwa sasa mkoa wa Dar es Salaam uko katika utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mipango Miji kwa hiyo utekelezaji wa mfumo wa wa anwani za makazi utaendana sambamba na mpango huo na utarahisisha zoezi la Sensa ya Makazi na Watu itakayofanyika Agosti mwaka huu”, alisema Makala.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.