POSTA KWA MAENDELEO YA UCHUMI WA TANZANIA
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari nchini Tanzania Dkt. Jim Yonazi amesema kuwa Sekta ya Posta ni muhimu kwa maendeleo ya uchumi wa nchi na dunia kwa ujumla kwasababu inawezesha usafirishaji wa mizigo popote duniani.
Hayo ameyazungumza wakati akifungua warsha ya watoa huduma ya usafirishaji wa mizigo na vifurushi nchini wenye leseni ya kufanya huduma hizo kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa lengo kujadili maendeleo na maboresho ya Sekta hiyo nchini hasa katika kipindi hiki ambacho Shirika la Posta Tanzania na wadau wake wanaadhimisha wiki ya Posta duniani.
Amesema kuwa Serikali imewekeza katika Sekta ya Posta ili kuhakikisha kunakuwa na miundombinu rafiki ya usafirishaji na ugavi huku akiitaja miundombinu hiyo kuwa ni pamoja na Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi ambazo hadi sasa halmashauri 21 nchini tayari zimeshafikiwa na muundombinu huo na mipango inaendelea kwa nchi nzima kufikiwa na
muundombinu huo.
Mfumo huo unaohusisha majina ya mitaa, barabara na namba za nyumba utawezesha na kurahisisha uchukuaji na ufikishaji wa mizigo pamoja na ufikishaji wa huduma mbalimbali kama zimamoto na polisi pale zinapohitajika.
Ameeleza kuwa kila kata sasa ina postikodi yake na zinatambulika katika mfumo wa postikodi na mwananchi anaweza kufahamu postikodi yake kwa kupiga *152*00# na kufuata maelekezo ambayo yatampatia namba ya postikodi ya eneo husika na kwa sababu namba hizi zinatofautiana zinarahisisha mhusika kufikiwa pale alipo.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt. Jabir Kuwe amesema Mamlaka hiyo imejiwekea utaratibu wa kukutana na watoa huduma wa Sekta ya Posta angalau mara mbili kwa mwaka kwa lengo la kujadili masuala yanayohusu Sekta hiyo nchini na kipindi hiki kinawaunganisha pamoja kuelekea maadhimisho ya Siku ya Posta Duniani.
Amesema kuwa katika kipindi hiki cha UVIKO 19, sekta nyingi ziliathiriwa na mlipuko wa UVIKO 19 ambapo kwa upande wa Sekta ya Posta baada ya kujikita na matumizi ya teknolojia imeendelea kuimarika kwa sababu mtu anaweza kuagiza bidhaa mtandaoni na Shirika la Posta likamsafirishia na kumfikishia mpaka mlangoni.
Ameongeza kuwa Serikali kupitia TCRA imeruhusu ushindani katika Sekta ya Posta ili kuboresha utoaji wa huduma, ubunifu na kuleta tija kwa taifa katika kukuza uchumi na kupunguza umasikini kwa kuyapatia leseni makampuni binafsi yanayofanya huduma za usafirishaji.
Post a Comment