DARAJA LA SUGUTI LAGHARIMU SHILINGI MILIONI 80
Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini(TARURA),Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Mhandisi Hussein Abbas amesema kuwa ujenzi wa Daraja la chuma la Suguti katika Mto Suguti umegharimu shilingi milioni 80 lenye urefu wa Mita 24 ambapo ujenzi wa Daraja hilo umepewa kipaumbele kwani ni muhimu kwa wananchi wa Suguti na Kataryo katika kupata mahitaji yao ya kila siku kwa kuwa wananchi hao wanategemea kupata huduma katika Kijiji cha Wanyere.
Kukamilika kwa ujenzi wa daraja hilo la Suguti ni sehemu ya mikakati ya TARURA ya kuboresha huduma ya usafiri na usafirirshaji hasa kwa maeneo ya pembezoni ambapo kwa mwaka wa fedha 2021/2022 Wakala umejipanga kuhakikisha unawafungulia huduma wananchi ili mahali maliposhindwa kufikika sasa pafikike na hii ni baada ya Serikali kuongeza bajeti ya Wakala.
Eneo hilo la Mto Suguti ilikuwa ni shida ya kuvuka kwenda upande wa pili hasa katika kipindi cha masika ambapo watoto walishindwa kwenda shule na akinamama wajawazito walishindwa pia kufika hospitalini kupata huduma, kwani mawasiliano huwa yanakatika kabisa.
Wananchi wa Kata ya Suguti walisema kuwa hapo awali kulikuwa na daraja la miti ambalo lilikuwa linahatarisha usalama wao hasa kipindi cha masika na kukatisha mawasiliano hivyo kushindwa kufika Wanyere ili kuweza kupata mahitaji yao na huduma za kijamii kama shule, hosptali na masoko.
“Tunaishukuru sana Serikali kwa ujenzi wa Daraja ili la Suguti sasa kwenda Kataryo si kikwazo tena watoto walikuwa wanashindwa kwenda shule hasa katika kipindi cha masika, tulikuwa hatuwezi kwenda upande wa pili na kusubiri maji yapungue hata siku tatu mpaka nne ndipo tuweze kwenda Wenyere kupata huduma za kijamii, kwa kweli tunaishukuru sana Serikali”, alisema Ndg. John Changulu mkazi wa Wanyere.
Post a Comment