MTANGAZAJI

WAZIRI AITAKA JAMII KUPINGA VIKALI UKATILI DHIDI YA WAZEE


Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto nchini Tanzania Dkt Doroth Gwajima amesema kuwa Serikali inakemea vikali na kupinga vitendo vya Ukatili dhidi ya wazee.

Waziri Dkt. Gwajima amewaambia waandishi wa habari  Jijini Dodoma wakati akitoa taarifa ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukatili dhidi Wazee yanayoadhimishwa Juni 15 kila mwaka.

Waziri Dkt Gwajima amesema kwamba Siku ya Kupinga Ukatili dhidi ya Wazee huadhimishwa ikiwa na lengo la Kulinda haki, Ulinzi na Usalama wa Wazee kama ilivyodhamiriwa kwenye azimio la Umoja wa kimataifa la mwaka 2011.
 
 Kwa mujibu wa taarifa ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa na vyombo vya habari kwa mwaka 2019 ilieleza kuwa kulikuwa wazee wengi Duniani kuliko watoto ambapo  watu wenye umri wa miaka 65 walikuwa ni  wengi ukilinganisha na wale walio chini ya miaka mitano mwishoni mwa mwaka 2018  huku idadi ikionesha kuwa kulikuwa na  watu takriban milioni 705 wenye miaka zaidi ya 65 duniani, wakati wale wenye umri kati ya miaka 0-4 ni takriban milioni 680

Dkt. Gwajima amesema Serikali inaendelea kutekeleza hafua mbalimbali za kuhakikisha ulinzi na usalama wa wazee wote hapa nchini ikiwa ni pamoja na kuratibu utekelezaji wa  Mkakati wa Kitaifa  wa Kutokomeza Mauaji ya Wazee 2018/19 – 2022/23.

Ameongeza kuwa katika kuhakikisha ulinzi na usalama wa wazee wasiojiweza na ambao hawana watu wa kuwatunza, Serikali inasimamia matunzo katika makazi ya wazee 13 yenye jumla ya wahudumiwa 262 (Me 163, Ke 100) na kuratibu huduma katika makazi 20 ya Taasisi za dini na watu binafsi yenye wahudumiwa 537 (Me 242, Ke 295) ambapo wazee hawa hupata huduma za chakula, malazi, mavazi, matibabu na msaada wa kisaikolojia na kijamii. 

Dkt.Gwajima amesema kuwa Serikali imeendelea kuwatambua na kuwapatia familia masikini wakiwemo wazee na kuwawezesha kupata mahitaji ya msingi kupitia mpango wa kunusuru kaya maskini unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), ambapo hadi kufikia Septemba 2019, jumla ya Wazee 680,056 (Wanaume 258,674 na Wanawake 421,382) wamenufaika na mpango huo

Aidha Waziri Dkt. Gwajima amesema kuwa Serikali inatambua kuwa wazee ni hazina ya taifa kutokana na ujuzi na uzoefu walio nao katika masuala mbalimbali ya kiuchumi na kijamii na katika kuhakikisha kuwa hazina hii inatumika ipasavyo, Serikali imeendelea na uundaji wa mabaraza ya wazee kote nchini. Jumla ya mabaraza 14,883 yameundwa kuanzia ngazi ya Vijiji/Mitaa, Kata, Wilaya na mikoa nchini.

Waziir Dkt. Gwajima ametoa wito kwa jamii kuhamasika katika kuhakikisha ulinzi na usalama wa wazee wote nchini. "

Tutumie siku hii katika kutafakari changamoto mbalimbali zinazowakumba wazee hapa nchini na kushirikiana kwa pamoja katika kuzitatua kama kauli mbiu ya mwaka huu inavyoelekeza". Alisisitiza Dkt. Gwajima.

Tarehe 15 Juni ya kila mwaka ni Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukatili dhidi ya Wazee na kwa mwaka huu Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukatili dhidi ya Wazee inaongozwa kwa kauli Mbiu isemayoTUPAZE SAUTI KUPINGA UKATILI DHIDI YA WAZEE.


No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.