AFRIKA YAONGOZA KWA IDADI YA WAADVENTISTA DUNIANI
Wakati kanisa la Waadventista wa Sabato likizindua mpango wa utume wa OneVoice27 duniani kote Septemba 5, mwaka huu. Kanisa hilo barani Afrika linaonekana kuchangia kwa zaidi ya asilimia 81 ya ongezeko la idadi ya washiriki duniani.
Kwa mujibu wa toleo la nane la Takwimu kwa mwaka 2026 lenye kurasa 22 lililotolewa na ofisi ya Kumbukumbu,takwimu na utafiti ya Kanisa hilo duniani linaonesha kuwa kanisa lilihitimisha mwaka 2025 likiwa na washiriki 24,372,139 duniani.
Takwimu zinaonesha kuwa Divisheni ya Afrika Mashariki na Kati (ECD) imeongeza zaidi ya washiriki 291,000, na kufikia karibu idadi ya washiriki milioni 6 katika eneo hilo lenye nchi 11 ambazo ni Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Djibouti, Eritrea, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Somalia, Sudan Kusini, Tanzania, na Uganda. Divisheni ya Afrika Kusini na Bahari ya Hindi (SID) imeongeza zaidi ya 208,000 na kufikia milioni 4.54. Huku Divisheni ya Afrika Magharibi na Kati (WAD) ikionesha ongezeko la washiriki karibu 61,000.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya idadi ya washiriki iliongezeka kwa washiriki 687,902 mwaka 2025. Ongezeko hilo ni dogo kuliko la mwaka 2024, huku ubatizo ukipungua kutoka zaidi ya milioni 1.51 hadi milioni 1.21.
Kwingineko, Divisheni ya Amerika Kaskazini (NAD) imeongezeka washiriki milioni 1.32, huku Divisheni ya Amerika Kusini na Inter-Amerika zikiripoti kupungua kidogo kwa idadi ya washiriki licha ya kurekodi zaidi ya ubatizo 294,000 kwa pamoja.
Takwimu hizi mpya zinakuja wakati Waadventista duniani kote wanazindua OneVoice27, mojawapo ya mipango mikubwa ya utume kimataifa iliyoanzishwa chini ya uongozi wa Kiongozi wa Kanisa hilo duniani Mchungaji Erton Köhler. Mpango huu uliwasilishwa kwa viongozi wa kanisa duniani kwa mara ya kwanza Oktoba 2025, na unalenga kuunganisha uinjilisti wa kidijitali, makanisa mahalia, na ushuhuda binafsi kuelekea msisitizo mkubwa wa uinjilisti mnamo Septemba 2027.
Uzinduzi wa Septemba 5 unalenga kuhamasisha angalau Waadventista milioni moja kushiriki maudhui yaliyobeba utume wa Kiadventista kwenye mitandao ya kijamii ukiwa na ujumbe wa jinsi Yesu anavyofanya “mambo yote kuwa mapya,” wakitumia hashtag ya #allthingsnew, #mamboyotemapya.

.png)
Post a Comment