SERIKALI YA TANZANIA KUZINDUA MAKAO YA TAIFA YA WATOTO WAISHIO MAZINGIRA HATARISHI
Kuelekea
Siku ya Mtoto wa Afrika, Serikali ya Tanzania inatarajia kuzindua Makao ya Taifa ya
Malezi na Makuzi ya Watoto yaliyojengwa katika Kata ya Kikombo, jijini
Dodoma.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia ,Wazee na Watoto nchini Tanzania, Dkt Dorothy Gwajima amewaambia Waandishi wa Habari jijini Dodoma kuwa Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Isdor Mpango atazindua
makao hayo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika
yatakayofanyika Juni 16 mwaka huu.
Dkt.
Gwajima amesema lengo la kujengwa kwa makao hayo ni kutatua changamoto
za makao ya Taifa ya awali yaliyokuwa Kurasini Dar es Salaam za ufinyu
wa maeneo ya shughuli mbalimbali ikiwemo michezo, bustani, ujasiriamali
na ufugaji kutofanyika sawasawa hivyo kufanya hali ya lishe na uchumi
kuwa duni.
"
Ujenzi huu ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa Taifa wa Kimkakati wa
kuwatambua, kutengamanisha na kuwaunganisha na familia watoto wanaoishi
katika mazingira hatarishi, pia ni utekelezaji wa maagizo ya Mhe. Rais
kuwa watoto wanaotunzwa kwenye makao waandaliwe mapema kadri
inavyowezekana kuwaunganisha na familia ili kuwawekea msingi wa malezi"
alisema Dkt. Gwajima.
Ameongeza
pia watoto wanatakiwa kukaa kwenye makao kwa muda tu na wakiisha
kuimarika warejeshwe kwenye makazi ya kawaida iwe ya kambo au kuasili
ili waishi kawaida katika familia.
Dkt.
Gwajima amesema, uzinduzi huo utaambatana na uzinduzi wa vituo vya
Jamii vya malezi, Makuzi na Maendeleo ya awali ya watoto pamoja na
Baraza la Taifa la Watoto juni 14 mwaka huu.
Aidha,
Dkt. Gwajima ametoa rai kwa wazazi na jamii kwa ujumla kuhakikisha
wanatimiza jukumu la malezi ya watoto wao na kuwa, hatua ya kulelewa
katika makao iwe ni ya mwisho baada ya hatua zote kushindikana.
Mradi
wa Ujenzi wa Makao ya Watoto Kikombo, umetekelezwa kwa Ushirikiano
kati ya Serikali kupitia Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia ,Wazee
na Watoto na Shirika la ABBOT Fund Tanzania na Makao hayo yana uwezo
wa kuhudumia watoto 250 kwa wakati mmoja na hadi sasa watoto
wanaohudumiwa katika Makao hayo ni 28.
Post a Comment