MTANGAZAJI

SERIKALI KUTANGAZA ZABUNI YA KUPELEKA MAWASILIANO MAENEO YA MIPAKANI

 
Serikali ya Tanzania kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) inatarajia kutangaza zabuni ya awamu ya sita yenye lengo la kupeleka mawasiliano katika kata 179 zenye vijiji 358 mradi unaolenga kupunguza changamoto ya mawasiliano kwa wananchi waishio mipakani.

Akizungumza katika kikao chake na watendaji wakuu wa makampuni ya simu kilichofanyika jijini Dodoma Juni  07,2021 Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari nchini Tanzania Dkt. Faustine Ndugulile amesema Mfuko huo utatangaza zabuni hizo mwezi huu kwa lengo la kuendelea kuboresha huduma za mawasiliano nchini.

“Kama Serikali tumejielekeza katika kuboresha mawasiliano ya mipakani ambayo
yanakuwa na mwingiliano na nchi za jirani, makampuni ya simu mkiwa kama wadau wa Sekta hii tunaomba mtoe ushirikiano kwa Serikali ili wananchi waishio mipakani wapate mawasiliano ya uhakika ya ndani ya nchi”, alisema Dkt. Ndugulile.

Katika hatua nyingine Dkt. Ndugulile ametoa rai kwa watendaji hao kufanya
maboresho ya utoaji wa huduma za mawasiliano kwa kufanyia kazi maeneo ambayo wananchi wanayalalamikia ikiwa ni pamoja na kuhakiki namba zilizosajiliwa kwa alama za vidole na kuimarisha mifumo ya usajili wa laini za simu pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa umma ili kupunguza utapeli kwa njia ya simu za mkononi.

Naye Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Mhandisi Kundo Mathew amesema Serikali ipo tayari kushirikiana na watoa huduma pamoja na watumiaji wa huduma za mawasiliano ili kuweza kutambua mahitaji halisi na changamoto zilizopo katika sekta hiyo na kuzitatua kwa lengo la kuendelea kuboresha Sekta hiyo muhimu nchini kwa kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma za mawasiliano popote alipo.

Kwa upande wa Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Justina Mashiba amesema kuwa lengo
la Mfuko huo ni kupeleka mawasiliano kwa wote na zabuni zitakazotangazwa mwezi huu ni kwa ajili ya kupeleka mawasiliano katika maeneo ya mipakani na kuyaomba makampuni ya simu kuchukulia zabuni hizo kwa uzito stahiki pindi
zitakapotangazwa.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.