MTANGAZAJI

WAZIRI AAGIZA KUKAMATWA MFANYABIASHARA

 

 Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) nchini Tanzania  Selemani Jafo ameagiza kukamatwa kwa Bw. Kaissy Mkurugenzi wa Kampuni ya Seif for Tobacco Trading Co. Ltd aliyeingiza nchini makontena zaidi ya mia tano (500) yenye malighafi ya Molasesi iliyoharibika na kuyatelekeza katika Bandari ya Dar es Salaam.

Waziri Jafo ametoa agizo hilo mara baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika Bandari ya Dar es Salaam na kushuhudia makontena hayo yakiwa yametelekezwa bandarini hapo na mengine kutawanywa katika baadhi ya bandari kavu jijini Dar es Salaam.

Amesema kamwe Tanzania haiwezi kugeuzwa kuwa dampo kwa kuruhusu bidhaa kutoka nje ya nchi ambazo muda wake wa matumizi umeisha kuingizwa nchini kwa lengo la kutupwa kiholela.

Imebainika kuwa mfanyabiashara huyo aliyetambulika kwa jina moja tu la Bw. Kaissy aliingia nchini kwa hati ya utembezi (tourist) na baadae kupatiwa kibali cha uwekezaji kupitia Export Processing Zone (EPZA) kilichomruhusu kuwekeza katika uzalishaji wa shisha kibali ambacho kilifutwa baada ya kugundulika kuwa kuna udanganyifu mkubwa kuhusu uwekezaji wake.

Aidha, Waziri Jafo amemwagiza Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa na Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Samwel Gwamaka kufanya ukaguzi katika Bandari kavu zote nchini kubaini bidhaa zilizoingizwa nchini zikiwa zimeisha muda wake wa matumizi ambazo zimetelekezwa kwa lengo la kuzitupa nchini na kuchukua hatua za kisheria.
 
Waziri Jafo amesema NEMC, TBS na Mamlaka ya Bandari ndani ya siku tatu
kuwasilisha taarifa ya kina kuhusu mwekezaji huyo na idadi kamili ya makontena yaliyoingizwa nchini na mfanyabiashara huyo.

“Kwa kuwa vipimo vilivyofanywa na TBS vinaonyesha kuwa Molasesi yote imekwisha haribika na ni hatari kwa afya ya binadamu na mazingira, namwagiza mfanyabiashara huyo kurudisha makontena hayo yalikotoka kwa gharama zake mwenyewe” Jafo alisisitiza.

Waziri Jafo pia ametembelea bomba za kusafirishia mafuta kutoka kwenye meli na kubaini uvujaji wa mafuta katika mabomba hayo unaosabishwa na uchakavu wa mitambo hiyo, Waziri Jafo ameagiza hatua za haraka kuchukuliwa kudhibiti uchafuzi wa Mazingira.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.