MWONGOZO WA KUKABILI UKATILI WA KIJINSIA VYUONI TANZANIA WAJA
Imeelezwa kuwa, Mwongozo wa uanzishwaji, uendeshaji na ufuatiliaji wa dawati la jinsia katika Taasisi za Elimu ya kati na Elimu ya Juu nchini Tanzania utasaidia kutatua changamoto za ukatili wa kijinsia zinazowakabili wanafunzi na wakufunzi vyuoni.
Hayo
yamebainika mkoani Dar es Salaam wakati wa kikao kati ya Serikali na
wadau kupitia Mwongozo wa uanzishwaji, uendeshaji na ufuatiliaji wa
dawati la jinsia katika Taasisi za Elimu ya kati na Elimu ya Juu .
Baadhi
ya Wadau wa masuala ya jinsia wakizungumza wakati wa kupitia rasimu ya
Mwongozo huo ulioandaliwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto, wamesema changamoto kubwa iliyokuwepo ni kukosekana
kwa mfumo mmoja wa kushughulikia matatizo ya ukatili wa kijinsia katika
taasisi za elimu.
Mmoja
wa wadau hao Dkt. Rose Shayo, mkufunzi mstaafu Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam amesema mwongozo huo ukikamilika na kuanza kutekelezwa utakuwa ni
moja ya silaha muhimu katika kupambana na vitendo vya ukatili vyuoni.
"Serikali
imefanya vyema kutushirikisha wadau kuandaa mwongozo huu ambao ni imani
yangu utaandaa mazingira mazuri kwa vyuo vyetu vya elimu ya juu na kati
kuwa na utaratibu mmoja wa kushughulikia masuala ya kijinsia tofauti na
hapo awali, kila Chuo kilikuwa na utaratibu wake" alisema Dkt Rose.
Nao
baadhi ya wanafunzi wa mwaka wa tatu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam Irene Paul na Joachim Peter wemesema kuwa, pamoja na kuwepo kwa
mifumo ya kushughulikia vitendo vya ukatili, bado vitendo hivyo
vinaendelea kushamiri ila wanaamini mwongozo utakapokamilika,
utawasaidia kuwa na nguvu zaidi ya kupambana na vitendo hiyo.
"Changamoto
za ukatili wa kijinsia zipo na zinachangia athari mbalimbali kwa
wanafunzi ikiwemo kukatisha masomo yao. Kuanzishwa kwa madawati haya
kutasaidia kwa kiasi kikubwa hasa kuwalinda watoa taarifa za ukatili
vyuoni, kwani kwa sasa wanafunzi wengi wamekuwa wakihofia usalama wao
hivyo kushindwa kutoa taarifa" alisema Irene.
Amesisitiza
kuwa, hatua zilizochukuliwa zitawasaidia kupunguza matatizo kwa wote
wanafunzi na wakufunzi kwani watajua njia sahihi na salama za kutoa
taarifa mahali husika.
Akifungua
kikao hicho Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Jinsia kutoka
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Grace
Mwangwa amewasisitiza wadau kuzingatia Mwongozo huo pale
utakapopitishwa kwani utawasaidia vijana pamoja na wakufunzi wa Taasisi
za Elimu ya kati na Elimu ya juu kupambana na vitendo vya Ukatili.
Mwangwa
ameongeza kuwa mwongozo huo unalenga kuhakikisha masuala yote ya
kijinsia yanaainishwa na kujumuishwa katika mipango kazi na Bajeti ya
taasisi hizo ili kuhakikisha changamoto za ukatili wa kijinsia
zinatatuliwa.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Women in Law and Development in
Africa (WiLDAF) Anna Kulayo amesema maandalizi ya Mwongozo huo
yamefanyika kwa muda mrefu hivyo ni wakati wa kuukamilisha ili ufanyiwe
kazi kwa lengo la kutokomeza vitendo vya ukatili kwenye Taasisi za Elimu
ya kati na Elimu ya Juu.
Post a Comment