MTANGAZAJI

MBUNGE ATAKA MAHAKAMA YA FAMILIA

 

Mbunge wa Viti Maalumu  Kupitia Asasi za Kiraia Tanzania Bara (NGOs) Neema Lugangira amesema ipo haja ya Serikali  ya nchi hiyo  kuanzisha Mahakama ya Familia yaani Family Court kama ilivyofanya kwenye Mahakama za Ardhi ili kusaidia kuondosha changamoto zinazojitokeza ikiwemo Masuala ya Matunzo ya Watoto.

Amesema ili Matunzo ya Watoto yaweze kubebwa kwa uzito unaostahili na kupanua wigo mpana wa haki ili kuhakikisha changamoto za namna hiyo zinaondoka kwenye jamii badala ya kuendelea kuwepo kila wakati.

Aliyasema hayo Bungeni Jijini Dodoma wakati alipouliza Maswali Mawili ya Nyongeza baada ya Serikali kuwasilisha Majibu ua Swali lake la Msingi lililouliza "Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwakomboa Wanawake wanaobebeshwa mzigo mkubwa wa kugharamia matunzo ya Watoto bila msaada wa Baba?" 

Mbunge Neema alisema pamoja na majibu mazuri ya Serikali lakini hata kwa Sheria zilizopo bado kuna changamoto kubwa kwenye eneo hilo.

Katika maswali yake ya nyongeza Mbunge Lugangira aliishauri Serikali iboreshe Sheria zilizopo ili gharama za matunzo ya watoto iendani na hali ya uchumi na maisha ya  sasa kutokana na maisha kuwa juu kuliko ilivyokuwa awali.

Akijibu Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto, Mwanaidi Khamisi amesema "Serikali imetoa maelekezo wazazi kuhakikisha mtoto anapata matunzo yote stahiki, na kama wazazi wa mtoto hawaishi pamoja na mtoto anaishi na Mama yake basi Baba atawajibika kugharamia malezi ya mtoto kulingana na kipato alichonacho". Swali hili pia lilimnyanyua Waziri Dkt Dorothy Gwajima ambae alisema "Nakiri tatizo Watoto kutelekezwa ni kubwa na ipo haja ya Serikali kufanya harakati za ziada ili kulidhibiti. 

Naibu Waziri Mwanaidi Ali Khamis alisema Serikali imekubaliana na ushauri wa Mbunge Neema Lugangira na ipo haja ya kuwa na chombo maalumu ambacho kitakuwa kinashughulikia masuala la familia hivyo wameupokea ushauri wa Mbunge Lugangira na wataufanyia kazi  kulingana na Sheria zilizopo.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.