MAJALIWA AWATAKA WATANZANIA KUSHIRIKI ZOEZI LA SENSA 2022
Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa ametoa wito kwa wananchi nchini humo kushiriki kikamilifu katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi linalotarajiwa kufanyika mwaka 2022 ili kuiwezesha Serikali kupanga maendeleo, kupunguza umasikini na kukuza uchumi.
Majaliwa ametoa rai hiyo jijini Dodoma wakati akizindua Kitabu cha
Mkakati wa Usimamizi wa Utekelezaji wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka
2022 kilichoandaliwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).
“Matokeo
ya sensa yataiwezesha Serikali kupata takwimu za msingi zinazotumika
kuakisi hali halisi iliyopo na kupanga mipango ya maendeleo kwa kutunga
sera pamoja na kupanga mipango, program na kufuatilia utekelezaji wake”,
alisema Mhe. Majaliwa.
Alisema
ni muhimu wananchi watoe ushirikiano kwa wakusanya takwimu ili
kuliwezesha zoezi hilo kuenda vizuri na kuleta matokeo tarajiwa kwa
maendeleo ya nchi.
Amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya nchini Tanzania kuanza kutoa elimu ya umuhimu
wa sensa kwa wananchi ili kuwaweka tayari kushiriki zoezi hilo muhimu
kwa maendeleo ya nchi hiyo.
Kwa
upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar, Hemed Suleiman Abdallah alisema kuwa kwa mujibu wa Katiba
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, sensa ya watu na
makazi ni miongoni mwa sehemu muhimu katika Muungano wa Tanzania.
Alisema
anaamini kuwa sensa ya mwaka 2022 itakuwa ya kipekee kutokana na juhudi
za viongozi na wataalamu waliopo ambao wamesha ainisha changamoto zote
zilizojitokeza katika sensa zilizopita na kupanga namna bora ya
kuzitatua kwa ajili ya kuboresha.
Naye
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango,Mhandisi Hamad Yussuf Masauni alisema Serikali inawajibu wa kuandaa zoezi la sensa ya watu na
makazi ili kupata idadi kamili ya watu na kuweza kupanga maendeleo ili
kukuza uchumi.
Alimhakikishia
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa kuwa Ofisi za Taifa za Takwimu za
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar zitahakikisha
zoezi hilo linafanyika kwa ufanisi mkubwa.
Awali
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba alisema
kuwa Uzinduzi wa Kitabu cha Mkakati wa Usimamizi wa Utekelezaji wa Sensa
ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 ni alama kuu ya uzinduzi rasmi wa
shughuli za maandalizi ya sensa hiyo ambayo majaribio yake yatafanyika
Agosti, 2021.
Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Alibina Chuwa alisema sensa ya watu na
makazi ya mwaka 2022 ni sensa ya sita kufanyika nchini ambapo sensa ya
kwanza ilifanyika 1967, ya pili 1978, ya tatu 1988, ya nne 2002 na ya
tano 2012.
Alisema
Sensa hiyo itakuwa ya kipekee kwa kuwa itatumia teknolojia ya hali ya
juu ili kupata taarifa kuanzia kwenye ngazi ya vitongoji, vijiji na
ngazi ya mitaa na mijini wakikusanya taarifa sahihi za idadi ya watu,
umri, elimu na upatikanaji wa huduma za kijamii kama maji, umeme na
afya.
Post a Comment