MTANGAZAJI

USHIRIKIANO WA TANZANIA NA IMF

 

Serikali ya Tanzania imeanza utekelezaji wa maelekezo ya kikao cha  Rais wa nchi hiyo Samia Suluhu Hassan na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha Kimataifa (IMF), Bi. Kristalina Georgieva kilichofanyika kwa njia ya mtandao mwanzoni mwa mwezi huu ambacho pamoja na mambo mengine walijadili kuhusu athari za kiuchumi na kijamii zilizotokana na changamoto za janga korona (Covid- 19).

Waziri wa Fedha na Mipango wa Tanzania Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba ametoa taarifa hiyo  alipokutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi Mkazi wa IMF nchini Tanzania, Bw. Jens Reinke katika ofisi za Wizara hiyo.

Amesema wamekutana ili kutafsiri maelekezo hayo katika utekelezaji ili kuiwezesha IMF kushirikiana na Tanzania katika kujenga uchumi ambao umekumbana na misukosuko inayoendelea Duniani inayotokana na  janga la Korona (Covid- 19).

Tumekutana na IMF pamoja na Wataalam wa Wizara pamoja na baadhi ya taasisi zake kujadili namna ya kuandaa taarifa ya maeneo yaliyoathirika zaidi na misukosuko hiyo pamoja na kuangalia kiwango cha athari katika maeneo husika”, alisema Dkt. Nchemba.

Dkt. Nchemba alisema athari za misukosuko hiyo ya uchumi zinatofautiana kisekta kwa kuwa kuna sekta ambazo zimeathirika moja kwa moja kama biashara, utalii na makusanyo, na kuna zile ambazo haziathiriki moja kwa moja.

Alisema wataangalia athari za misukusuko hiyo katika huduma za jamii kwa upana wake kama huduma za Afya hususani kuboresha miundombinu, dawa na upatikanaji wa vifaa tiba pamoja na suala la upatikanaji wa maji.

Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa IMF nchini, Bw. Jens Reinke alisema shirika hilo lipo tayari kushirikiana na Tanzania na kubainisha kuwa yeye binafsi yupo tayari kufanya kazi na wataalam wa Tanzania ili kusaidia nchi na kuhakikisha uchumi wa nchi unakuwa kwa kasi kama ilivyopangwa.


No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.