KANUNI NA SHERIA ZA VYOMBO VYA HABARI TANZANIA
Waziri anayesimamia Sekta ya Habari nchini Tanzania Innocent Bashungwa na Waziri anayesimamia Sekta ya Mawasiliano Dkt. Faustine Ndugulile na timu ya Makatibu Wakuu na Wataalam wa Wizara hizo wamekaa na kujadili hoja mbalimbali kuhusu utekelezaji wa Sera, Sheria na Kanuni za kisekta kufuatia maelekezo ya hivi karibuni ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Majadiliano hayo yamefanyika jijini Dodoma Aprili 14, 2021 na kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukuliwa kwenye hoja 13 zilizoainishwa na Wizara hizo kufuatia wakati wa kuwaapisha Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu na Wakuu wa Taasisi ya kufanya marekebisho ya Sheria na Kanuni zinazosimamia Vyombo vya Habari hususan Televisheni Mtandao (Online TV).
Miongoni mwa maazimio yaliyofikiwa ni pamoja na kufanya mapitio ya Sera, Sheria,Kanuni na Miongozo katika maeneo yote yenye mapungufu ili ziendane na hali halisi ya sasa na kuweka mifumo rafiki ya kushughulikia masuala yote yanayohusu sekta ya Mawasiliano na Utangazaji.
Pia, Wizara zimeaazimia kuja na mkakati wa kuwaelimisha wadau wa Sekta hizo ili kudhibiti makosa ya kimaudhui yanayofanywa na Vyombo vya Habari badala ya hali ilivyo sasa inayotoa adhabu kali zinazojikita kwenye utozaji wa faini kubwa pamoja na kufungiwa.
Suala lingine ambalo limeazimiwa kufanyiwa kazi ni chaneli za bure kutoonekana kwenye visimbusi ambavyo kimsingi zinapaswa kuonekana hata pale kifurushi kinapokuwa kimeisha muda wake.
Post a Comment