MTANGAZAJI

TANZANIA KUTOA TIBA KWA NJIA YA MTANDAO

 

Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote nchini Tanzania (USCAF) umesema umeanza kutekeleza  mradi wa tiba mtandao huduma ambayo itawawezesha madaktari bingwa walio katika hospitali za mijini kutoa huduma kwa njia ya mtandao kwa wananchi wanaoishi maeneo ya Vijijini na pembezoni mwa Tanzania.

 Afisa Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Justina Mashiba ameeleza mpango huo wakati
alipowasilisha taarifa ya majukumu ya UCSAF katika semina ya kuwajengea uwezo wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu iliyofanyika  Dodoma.

Mpango huo unaonesha kuwa huduma ya kimtandao itaunganisha hospitali zilizoko mijini na zile za vijijini na pembezoni ili wananchi katika maeneo hayo waweze kupata huduma za madaktari bingwa wakiwa katika maeneo yao pasipo kusafiri kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na vipimo mbalimbali vya kiafya.


“Kwa huduma hii mtu aliyeko Kigoma hatalazimika tena kusafiri kwenda Muhimbili, tunataka teknolojia itusaidie ili kwamba daktari aliyeko Muhimbili aweze kumtibu mgonjwa aliyeko pembezoni” alisema Mashiba


Humphrey Polepole ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za
Mitaa ambaye pia alishiriki semina hiyo, ameipongeza UCSAF kwa kujenga vituo vya TEHAMA Visiwani Zanzibar ikiwa ni moja ya utekelezaji wa miradi yake huku
akishauri kuwa vituo kama hivyo vijengwe pia Tanzania Bara.

 Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote ulianzishwa kwa Sheria ya Bunge namba 11 ya
mwaka 2006 Sura ya 422 kwa lengo la kufikisha huduma za Mawasiliano ya simu,
Radio, Runinga pamoja na huduma za Posta katika maeneo ya Vijijini na Mijini kusiko na huduma hiyo au yenye mawasiliano hafifu.


Hadi sasa Mfuko umefikisha  huduma mbalimbali za mawasiliano ikiwa ni pamoja na kuwasha minara katika kata 633 zenye vijiji 2,320, kuunganisha mtandao wa intaneti na kutoa vifaa vya TEHAMA kwa shule 711, kutoa mafunzo ya TEHAMA kwa walimu 2,213 wa shule za UMMA kutoka Mikoa yote ya Tanzania Bara pamojana kujenga vituo 10 vya TEHAMA visiwani Zanzibar.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.