MKONGO WA TAIFA WA MAWASILIANO WAUNGANISHA VISIWA VYA UNGUJA NA PEMBA
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimeweka saini ya mkataba wa makubaliano wa kuunganisha visiwa vya Pemba na Unguja na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na Mkongo wa Zanzibar.
Utiaji saini huo umeshuhudiwa na katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Dkt. Zainabu Chaula wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Dkt. Mustafa Aboud Jumbe, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Utiaji saini huo umefanywa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Waziri Kindamba kwa upande wa Bara na Mhandisi Shukuru Awadh Suleiman, Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Miundombinu ya TEHAMA Zanzibar (ZICTIA) kwa upande wa Zanzibar.
Kabla ya kushudia tukio hilo, Dkt. Zainabu Chaula alisema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejenga Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 700 na kuunganisha kwenye mikoa yote 26 ya Tanzania Bara na kwenye nchi jirani za Congo, Zambia, Rwanda, Burundi, Kenya, Uganda na Malawi ambapo maunganisho haya yanaenda kufungua fursa za wawekezaji na watumiaji wa huduma za mawasiliano wa ndani na nje ya Tanzania kuunganishwa na Zanzibar kwa kuwa katika kipindi cha miaka mitano tumeshuhudia kuibuka kwa mifumo ya TEHAMA ambayo inawezesha utoaji wa huduma za mawasiliano kwa wananchi kwa sasa.
Dkt. Jumbe amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar SMZ imetumia zaidi ya shilingi bilioni 30 kuunganisha mikoa na wilaya zote za Unguja na Pemba bali kulikuwa na changamoto ya kuunganisha Unguja na Pemba ila sasa kwa kupitia makubaliano hay0, watatumia barabara ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kuunganisha visiwa Pemba na Unguja na hivyo Zanzibar kuunganishwa na Tanzania Bara moja kwa moja na utawezesha kupunguza gharama za mawasiliano ili ziwe nafuu.
Ndugu Kindamba amesema kuwa ufunguzi wa njia za mawasiliano ya Mkongo kati ya Tanzania Bara na Zanzibar utakuwa na manufaa makubwa sana kwa taifa hasa katika kuwezesha kuongezeka kwa matumizi ya data na intaneti na makubaliano hayo yanahusisha kutunza vifaa vya miundombinu ya TEHAMA vya ZICTIA kwenye majengo ya TTCL.
Mhandisi Suleimani ameongeza kuwa ZICTIA imekamilisha ujenzi wa Mkongo wa Zanzibar na sasa unaunganishwa na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ambapo itakuza na kuongeza huduma za mawasiliano; kuondoa changamoto iliyokuwepo Zanzibar ya kutumia njia ya mawasiliano ya mawimbi ya radio kutoa huduma za mawasiliano ambayo hayana kasi na ubora unaohitajika, kupunguza gharama za mawasiliano na kuingizia mapato kwa Serikali
Post a Comment