DODOMA:SHEREHE ZA KUKABIDHI KATIBA ILIYOPENDEKEZWA KUFANYIKA KESHO
Sherehe za kukabidhi Katiba inayopendekezwa kwa Rais
Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein itafanyika kesho
kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
Sherehe hiyo
itakayoanza saa 6:00 mchana itahudhuriwa na marais wastaafu wa Zanzibar na Tanzania Bara,mabalozi
wanaoziwakilisha nchi zao nchini , viongozi wa ngazi tofauti wa kitaifa, watu
mashuhuri na wawakilishi wa makundi yote ya jamii ya Watanzania, ambayo
yameguswa na katiba hiyo inayopendekezwa.
Oktoba 2
mwaka huu Bunge maalumu la
Katiba nchini Tanzania lilipitisha rasimu ya katiba iliyopendekezwa,hatua hiyo
ilifikiwa baada ya kura za ndio zilizopigwa na wajumbe kufikia kiwango
kinachostahili, ili katiba hiyo iliyopendekezwa ipite ilitakiwa kuungwa mkono
na kura za ndio theluthi mbili kutoka Tanzania bara na theluthi mbili za ndio
kutoka Zanzibar.
Jumla ya wajumbe wote wa bunge hilo la Katiba
ni 629, huku 419 wakitoka Tanzania bara na 210 kutoka Zanzibar.
Zoezi hilo la upigaji kura ambalo lilianza
Septemba 29 mpaka Oktoba 2, siku matokeo yalipotangazwa, lilisusiwa na wabunge
wengi wa upinzani, kwa madai kuwa baadhi ya vipengele vya awali
vilivyopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyopewa kazi ya kukusanya
maoni kutoka kwa mwananchi, vilikuwa vimeondolewa.
Rasimu hiyo ya katiba ilipendekezwa na kamati
ya uandishi kuwa na jina la KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA YA MWAKA
2014 .
Post a Comment