SARAFU MPYA YA SHILINGI 500 KUANZA KUTUMIKA TANZANIA OKTOBA 2014
Benki
Kuu ya Tanzania imetoa toleo jipya la sarafu ya shilingi 500
itakayoanza kutumika Oktoba 2014 itakayokuwa mbadala wa Noti ya shilingi
500 inayoonekana kuchakaa haraka.
Hayo
yamesemwa leo Jijini Dar es salaam na Mkurugenzi wa Huduma za kibenki
wa benki hiyo Bw. Emmanuel Boaz wakati wa mkutano na waandishi wa
habari.
“Noti
ya shilingi 500 hupita kwenye mikono ya watu wengi zaidi na ndiyo
inayotumika zaidi kwenye manunuzi ya kawaida hivyo kuchakaa haraka ndio
maana tumeamua kutoa toleo la sarafu itakayoanza kutumika mapema mwezi wa 10 mwaka huu.”alisema Boaz.
Akifafanua
zaidi Boaz amesema Sarafu hukaa kwenye mzunguko kwa miaka mingi zaidi
kuliko noti na pia noti zimekuwa zikikaa katika mzunguko kwa muda mrefu
bila kurejeshwa kwenye mabenki kwa wakati muafaka ili zibadilishwe.
Akitaja
sifa za sarafu hiyo mpya Boaz amesema kwanza umbo lake ni la duara
lenye michirizi pembezoni na kipenyo cha milimita 27.5 na uzito wa gramu
9.5.
Sifa nyingineni
kuwa ina rangi ya fedha na imetengenezwa kwa madini aina ya chuma na
Nickel na kwa upande wa mbele ina sura ya Rais wa kwanza wa Serikali ya
mapinduzi ya Zanzibar sheikh Abeid Aman Karume na kwa nyuma ina taswira
ya mnyama nyati akiwa mbugani.
Pia
Boaz alibainisha kuwa sarafu hiyo kwa upande wa nyuma ina kivuli
kilichojificha ambacho huonesha thamani ya sarafu ya 500 au neno BOT
inapogeuzwa geuzwa.
Kwa
upande wa matumizi Boaz amesema sarafu hiyo itakapoanza kutumika
itatumika sambamba na noti za shilingi 500 hadi zitakapokwisha kwenye
mzunguko.
Benki Kuu ya Tanzania ndiyo chombo chenye jukumu la kutoa sarafu na noti halali (legal tender) zinazotumika nchini ambapo katika kutimiza jukumu hili Benki kuu hutengeneza noti na sarafu zenye uwiano mzuri wa thamani (denomination) unaozingatia uwezekano wa zile zenye thamani kubwa kuweza kugawika katika zile zenye thamani ndogo.(Chanzo:Wanabidii)
Post a Comment