MTANGAZAJI

MANYARA:ASKARI WA KAMPUNI YA TANZANITEONE WALALAMIKIWA KWA KUPIGA WAFANYAKAZI


Wachimbaji wa madini ya Tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wamelalamikia kitendo cha askari wa kampuni ya TanzaniteOne kuwapiga wafanyakazi na  kupora dhana  zao kwa madai ya kuwaingilia migodini mwao.

Wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti, wachimbaji hao wamedai kuwa walinzi wa kampuni hiyo ambayo hivi sasa ina hisa asilimia 50 kwa 50 na Serikali wamekuwa wakiingia bila idhini kwenye migodi wanayopakana nayo na kufanya matukio kama hayo.

Kwa upande wake mmoja kati ya wamiliki wa mgodi wa eneo hilo la kitalu B (Opec), Mohamed Karia amesema juzi walinzi wa kampuni hiyo waliingia chini mgodini kwake  na kupora mashine mbili za kuchorongea mgodi (Diga) na kuwajeruhi walinzi  huku akidai kuwa amechimba mgodi huo kwa muda mrefu na hakuwahi kuandikiwa barua yoyote ya onyo na Wizara ya Nishati na Madini, hivyo anashangazwa na kitendo hicho cha ukatili kilichofanya na kampuni hiyo.

Hata hivyo, Ofisa uhusiano wa kampuni ya TanzaniteOne Halfan Hayeshi amesema walinzi wa kampuni hiyo hawajawahi kuingia kwenye mgodi wowote wa mchimbaji mdogo na kufanya tukio lolote lile la kiualifu.

Kwa upande wake, kamanda wa polisi wa mkoa wa Manyara, SACP Deusdedit Nsimeki, amesema Karia alifika polisi na kutoa taarifa juu ya tukio hilo ambapo  wanaendelea na uchunguzi juu ya tukio hilo na watatoa taarifa.


No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.