MCH.JOKTAN MUURA NG'OMBOLI KUYENGA KUZIKWA LEO HUKO MOROGORO
Marehemu Mch Joktan Kuyenga (watatu toka kulia)enzi za uhai wake akifuatiwa na mkewe ambaye pia ni marehemu |
( MACHI 10, 1931 – NOVEMBA 7 2013) atazikwa leo mjini Morogoro ambapo huduma maalum yake mazishi itakayofanyika eneo la Misufini, Morogoro, ndani ya viwanja vya makao makuu ya Jimbo la Mashariki mwa Tanzania, ETC, kuanzia majira ya saa asubuhi.
HISTORIA FUPI YA MAREHEMU, MCHUNGAJI
“Yeye maisha yake yote aliamua kuwa Mcha-Mungu, na sisi sote tukamfahamu kuwa hivyo katika msimamo wake. Amekuwa mshauri wangu wa pekee; siyo mimi tu, hata kwa wanafamilia wote. Kwa kweli tutazikosa busara zake”. Aliyatamka hayo Mch. Donald Mnyerwe Kuyenga, mdogo wake marehemu, ambaye yeye anaendelea kuhudumu kama Mchungaji-mstaafu wa Kanisa la Mennonite Jimbo la Mara.
Marehemu Mchungaji Joktan Muura Ng’omboli Kuyenga alizaliwa Machi 10, 1931 kule Butata, na kukulia Murangi, Majita. Kama Mukome wa kweli, aliweka msimamo wa maisha yake mapema, na kutetea hiyo haiba maisha yake yote.
Elimu Ya Awali
Akiwa na umri wa miaka 16, Joktan alidhamiria kubadili maisha yake ya uvuvi na ukulima, na kutafuta kuwa Mwalimu na Mwinjilisti. Alipoomba kujisajili darasa la kwanza, Afisa Elimu wa Wilaya alimjibu, “Rudi nyumbani; wewe umeshazeeka”. Huyu Mkome hakuwa mtu wa kukatishwa tamaa. Alihamia Murangi Bush School mahali alipoanza darasa la kwanza na la pili mwaka 1947 – 1948. Darasa la tatu hadi la sita aliendelea kujisomesha mwenyewe pale Bwasi Central School, huku akilima pamba pamoja na wadogo zake ili kujilipia ada. Mwaka 1951 – 1952 alikwenda Ikizu Teachers’ Training School kukamilisha darasa la saba na nane.
Joktan alipata kujiendeleza kwa mafunzo ya Uinjilisti ya Special Secondary. Kwa wale waliokuwepo Ikizu kipindi hicho, naam, na wale tuliosimuliwa habari zake, twafahamu kuwa Joktan alionyesha msimamo wa dhati kwa haki, akikemea uonevu wa kikoloni hata ndani ya shule za Misheni. Anakumbukwa kama mwanafunzi mtanashati, mwadilifu, na kiongozi katika kutetea watu weusi.
Kazi na Ndoa
Akiwa kapera mtanashati na Mwalimu/Mwinjilisti mwenye umri wa miaka 28, mwenye kisomo cha kutamanika, na mwenye kutumia kisu na umma alapo chakula, Joktan alikuwa kivutio kwa waseja wengi. Hata hivyo, hakubahatika kumpata aliyemridhisha yeye na vigezo vyake vya kipekee. Alianza kazi kama Mwinjilisti wa Mtaa wa Musoma, akingali kapera. Miaka miwili iliyofuatia (1960 – 1961), Mwinjilisti Joktan Kuyenga alitumwa kama Mwalimu Mkuu wa Bwasi Primary School. Wadhifa huo ulikuwa umehifadhiwa kwa walimu wenye “Grade A”, lakini ilidhihirika kwamba Joktan, japo ni mhitimu tu wa darasa la 10, angemudu vema majukumu ya wadhifa huo. Haikuchukuwa muda kwa Joktan kujishawishi kwamba alihitaji kujiendeleza, uamuzi uluiompeleka Bugema Ministerial College, Uganda, mwaka 1961 – 1963. Akiwepo hapo, alifukuzwa shule kwa kilichodaiwa kuwa ni ukaidi wa kukataa maagizo ya Mkuu wa shule na viongozi wengine wa kazi. Hatimaye ilibainika kwamba wanachuo hao hawakuwa hatiani, na hivyo kumrejeza masomoni yeye pamoja na Wainjilisti wenzake Watanzania. Walikuwa radhi kutendwa hiana, alimradi walibaki kuwa waaminifu kwa dhamira zao, na Mungu wao. Naye Mungu hakuwaacha hadi walipohitimisha mafunzo ya Umishenari na Uchungaji mwaka 1963.
Kapera Joktan alikubali kutekwa katika penzi lake Mary Weseja Mirobho (ambaye amemtangulia kwa mauti tangu Juni 15, 2012). Kwa kulima pamba na kuuza, Joktan alijitafutia mahari, na kumwezesha kufunga pingu za maisha na mchumba wake tarehe 15 Januari, 1963. Mchungaji Daniel Yangwe Mutani (Marehemu) aliendesha huduma takatifu ya ndoa.
Kama zilivyo ahadi Zake, Bwana aliibariki hii ndoa kwa watoto.
• Kweli Kuyenga alizaliwa mwaka 1964 wakiwa Mgomeni, Dar es Salaam, kama Mchungaji wa Mtaa. Hata hivyo, huyu mzaliwa wa kwanza kabisa aliwatangulia wote katika mauti akingali mtoto mchanga.
• Heri Gideon Kuyenga alizaliwa mwaka 1965, wakiwa Misufini, Morogoro katika mafunzo ya kimataifa ya Kilimo cha Kisasa cha bustani na mboga-mboga. Mafunzo haya yaliendeshwa kama sehemu ya mafunzo kwa Wainjilisti na Watumishi wa kanisa.
• Deborah Nyamujungu Kuyenga alizaliwa mwaka 1966 pale Magomeni, Dar es Salaam, wakiwa kama Mchungaji wa Mtaa huo.
• Kulindwa Harun Kuyenga alizaliwa mwaka 1968 wakiwa Bwasi, Majita kama Mkurugenzi wa Vijana, Shule ya Sabato, na Huduma katika Field hiyo.
• Michael Magesa Kuyenga alizaliwa mwaka 1971, wakingali Bwasi katika utumishi huo huo.
Pamoja na hao watoto wanne, Mtumishi wa Mungu ameacha pia wajukuu wanane.
Utumishi wa Kichungaji
Mchungaji Joktan Kuyenga aliwekewa mikono ya Huduma ya Uchungaji katika Kanisa la Waadventista wa Sabato Ulimwenguni siku ya Jumamosi, tarehe 27 Januari, 1968, pale Ikizu Seminary. Wachungaji wahudumu walikuwa Mch. Elizaphan B Wanjara, Mch. Yohana Lusingu, na Mch E Olsen.
Utumishi wake kama Mwalimu Mkuu wa shule za Misheni, Mwinjilisti, na kiongozi wa Idara katika Fildi mbalimbali za Kanisa nchini Tanzania ulimpatia Joktan uzoefu wa kiroho na uhodari katika utumishi. Mwaka 1972 – 1978 alifahamika katika Kanisa la Waadventista wa Sabato nchini Tanzania na nje pia kama Kamanda wa Vijana. Aliinua Idara ya Vijana Tanzania Union (ikiwa Busegwe, Mara), na kuwapatia staha iliyowastahili vijana waliojulikana kama Missionary Volunteers (MV).
Mwaka huo, kwa nia yake ya kujiendeleza, Joktan aliuza vyote alivyokua navyo na kujipeleka nchini India kwa elimu ya juu katika Chuo Kikuu kule Spicer Memorial College. Baadhi walimdhihaki kwa kusema yawezekanaje mtu mwenye cheo kikubwa, umaarufu mkubwa, na jina kubwa, aache vyote hivyo kwa ajili ya kujitaabisha na elimu. Lakini Mkome alikata shauri, na “kuishika sana elimu, tena bila kuiacha”. Alikamilisha shahada yake katika Theolojia, na kurejea nchini pamoja na familia yake mwaka 1984. Mchungaji Kuyenga alitumika Temeke, Dar es Salaam kama Mchungaji wa Mtaa, kabla ya kupokea majukumu makubwa zaidi ya kuwa Kiongozi (President) wa East Tanzania Field (sasa Eastern Tanzania Conference – ETC) mwaka 1986. Walitenda kazi ngumu hususani maeneno ya kusini mwa Tanzania pamoja na Mch. Fadhili Manento kama Katibu, na Mzee Mavanza kama Mhazini, hadi Joktan alipohamishwa kwenda kwa wadhifa huo huo kule South-West Tanzania Field (sasa Southern Highlands Conference). Kule Mbeya, Mchungaji Joktan alishirikiana na Ndg Randa (marehemu), pamoja na Ndugu Zablon Masele katika Ofisi Kuu.
Mwaka 1996, Mchungaji Kuyenga alichaguliwa kusimamia kitengo cha Sauti ya Unabii (VOP) kilichopo Misufini, Morogoro, kama Mwalimu wa Biblia. Hata hivyo, alishika wadhifa huo kwa muda wa wiki moja tu, kabla ya kuhamishwa kwenda Makao Makuu ya Union ya Tanzania tena (wakati huu yakiwa Njiro, Arusha) kama Mkurugenzi wa Idara za Huduma, Wachungaji, na Wanawake.
• Akiwa amewasomesha watoto wake wote (pamoja na malezi kwa wajukuu), na pia kuwaoza na kuozesha hao watoto…
• Akiwa amedumu pasipo kuterereka kokote kule kwa ndoa yake ya miaka 49 na kipenzi cha ujana wake…
• Akiwa ametumika kwa uaminifu pasipo kashfa yoyote ile katika ngazi zote za uongozi katika utumishi wa kanisa nchini Tanzania na nje…
• Akiwa amekuwa kielelezo cha usafi kwa vijana na kimbilio kwa mashauri kwa walio wazee na wenye shida…
• Akiwa amekamilisha ujenzi wa makazi yake uzeeni na kujipatia heshima kwa watumishi wenzake na waliokuwa chini yake katika utumishi…
• Akiwa amepigana vita vilivyo vizuri katika utumishi shambani Mwake Bwana, na kuitetea imani ya Kikristo kwa wana-ndugu, majirani, na wasiomcha Mungu iwe mimbarani ama mashambani…
• Akiwa amekubalika na mbingu kama “mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, akitumia kwa halali neno la kweli”…
• Akiwa ametenda haya, naam na zaidi sana ya haya, kuwa shujaa wa msalaba Wake Kristo, asiyeionea haya Injili…
Baada ya hayo, Mchungaji Joktan Muura Kuyenga alistaafu utumishi na ajira ya kanisa mwezi Desemba, mwaka 1998.
Hata hivyo, hakustaafu utumishi shambani mwa Bwana. Aliendelea kuhudumia makanisa ya Mazimbu na Kihonda mjini Morogoro kama mchungaji wao, mahali alipokuwa ameweka makazi yake ya uzeeni. Huduma yake ya Kikristo ililipwa hapa hapa duniani na waumini waliomlea yeye na familia yake hapo Kihonda. Washiriki na majirani walimrudishia wema kwa wema. Kwa kila fadhila aliyowakirimu, wao walimlipa kwa fadhila kubwa zaidi, pasipo wao wenyewe kujitambua kwamba walikuwa wakitenda hilo kama malipo ya Mwenyezi Mungu kwa mchaji Wake.
Mauti
Japo alijulikana kama “Chuma cha Mjerumani” kiafya, hali ya Mch. Joktan Kuyenga ilizorota kwa ghafla na kwa kasi sana baada ya kifo cha mkewe, Mary, mwaka 2012. Msongo uliotokana na kumkosa huyu mpenzi wake wa miaka takriban 50 uliibua hali za magonjwa ambazo hazikuwahi kuwepo hapo awali. Ni hakika madaktari watakuwa na maelezo yakinifu zaidi kuelezea kile kilichosababisha mauti akiwa ndani ya chumba cha matazamio makuu (ICU) katika Hospitali ya Mkoa Morogoro.
Hata hivyo, tunafarijika kufahamu kwamba Marehemu Joktan Muura Ng’omboli Kuyenga amepumzika kidogo katika mauti, huku akiwa na wimbo wa matumaini kinywani na moyoni mwake: “Furaha Kwa Ulimwengu, Bwana Atakuja!”
Mauti amempumzisha shujaa wa Imani Joktan Muura Kuyenga. Mauti amembembeleza jemadari Wake Kristo Joktan Muura Kuyenga kulala usingizi. Mauti amemhifadhi kamanda wa vita ya Wema dhidi ya Uasi Joktan Muura Kuyenga mafichoni tusimwone…
LAKINI, “Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza. Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele. Basi, farijianeni kwa maneno hayo”. (1 Wathesalonike 4: 16 – 18)-Imeandikwa na aliyewahi kuwa Meneja wa kwanza wa Morning Star Radio,Mch Michael Kuyenga ambaye ni mtoto wa marehemu
Post a Comment