MTANGAZAJI

TAMKO LA JUKWAA LA WAHARIRI KUHUSU KUSUDIO LA KUZUIWA KWA MATANGAZO YA MOJA KWA MOJA BUNGENI

UTANGULIZI
1.   JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF) limepokea kwa masikitiko taarifa kwamba Bunge linaandaa utaratibu wa kuzuia vyombo vya habari kurusha moja kwa moja (live) matangazo ya Bunge.

2.   Taarifa ya Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah aliyoitoa juzi Jumatano, Februari 13, 2013 inasema kwamba eti ni kosa pia kwa wapigapicha kuwapiga picha wabunge wakiwa wamesinzia ndani ya ukumbi wa bunge.

3.   Kwamba baadhi ya wabunge wanazomoka kwa kujua kwamba michango yao inarushwa moja kwa moja hewani na hivyo kufanya vituko bungeni, kwahiyo kuzuia matangazo ya moja kwa moja ni kuwadhibiti wale wanaofanya fujo na vituko Bungeni.

4.   Dk. Kashililah anasema kwamba ofisi yake inaandaa mpango wa kurekodi vipindi hivyo na kuvirusha baadaye vikiwa vimehaririwa na kwamba ofisi yake inawasiliana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kupata njia ya kurusha matangazo hayo ya Bunge yaliyohaririwa.

MAONI YA TEF
Hatua hii ya ofisi ya Bunge inatupa shaka na pengine ni ishara ya mwendelezo ya kile ambacho kinaonekana kama jitihada mpya za kuuminya uhuru wa habari nchini. Kwa maana hiyo;
   
1.   Tunashangaa Bunge la Tanzania limejifunza wapi siasa hizi za kufunika mambo yanayowahusu wananchi, huku likijua kwamba wanaofuatilia vikao hivyo ndio walipa kodi na wapiga kura wa wabunge ambao uongozi wa Bunge unataka kuwalinda?

2.   Ni kama Taifa letu linarudi katika enzi za giza la usiri ambao kimsingi hatupaswi kuurejea. Tangazo hili ni moja ya mambo ya bahati mbaya yanayoikuba nchi yetu kwa sasa, wakati ambao dunia inahimiza uwazi hasa katika vyombo vya uamuzi.

3.    Ikumbukwe kwamba Tanzania imetokea katika mfumo wa chama kimoja kilichoshika hatamu hadi 1992, ambao uliifanya Serikali, Bunge na Mahakama kuendeshwa kwa usiri wa hali ya juu.

4.   Mara zote, usiri ni chimbuko la matumizi mabaya ya madaraka ni kinyume na misingi ya utawala bora na usiri unatoa mamlaka yasiyositahiki kwa kikundi cha watu wachache wenye masilahi binafsi ya kufisadi nchi.

5.   Hali hii inatufanya tuwe na shaka iwapo serikali yetu ilifanya kwa dhati mambo yafuatayo:
(a)                Kuridhia Tamko la Haki za Binadamu, Desemba 10, 1948 ambapo Kifungu cha 19 cha tamko hili (Article 19) kinatoa uhuru wa mtu kutoa na kupokea mawazo bila kujali mipaka ya nchi na haki hii ya kutoa mawazo haipaswi kuingiliwa.

(b)                Kufanya mabadiliko ya 5 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1984 ambayo kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hii, yaliliingiza tamko hili la Haki za Binadamu hivyo kuwezesha Ibara ya 18 ya katiba hiyo ya 1977 kuakisi Kifungu cha 19 cha tamko hiko kwa kutoa uhuru mawasiliano na haki ya kupewa taarifa.

(c)               Kutia saini Mpango wa Sherikali ya Uwazi (Open Government Partnership/Initiative) unaongozwa na Rais Barrack Obama wa Marekani mwaka 2010, ambapo tayari Wizara ya Katiba na Sheria imeanza mchakato wa kutunga Sheria ya Haki ya Kupata Habari, itakayoruhusu nyaraka zote muhimu za Serikali kuwekwa wazi kwa wananchi.

SIMAMO WA TEF
1.   Tunautaka uongozi wa Bunge kuachana  na harakati hizo kwani hazitasaidia kukuza demokorasia au kuboresha maadili ya Bunge. Badala yake zitazidisha mashaka ya umma dhidi ya chombo hicho cha uwakilishi kwa wananchi kutaka kufanya kazi zao “gizani”.

2.   TEF tunamaani kwamba kazi ya utangazaji si kazi inayopaswa kusimamiwa na uongozi wa Bunge, wala hatuna kumbukumbu za matukio na hatua za namna hii katika miaka ya karibuni, hata katika nchi  nyingine.

3.   Ikumbukwe kuwa, kama si ufinyu wa nafasi na mfumo wa uwakilishi bungeni tunaoutumia, ilibidi wananchi wote waingie bungeni na kutoa mawazo yao. Kwa maana nyingine wabunge ni wawakilishi wa wananchi na hivyo ni dhambi kuweka usiri wa yale yanayozungumzwa au kuhariri alichozungumza mbunge aliyetumwa na wananchi.

4.   Tunaamini kwamba jitihada zozote za kuwafungia wabunge ndani na kuhariri kazi wanazofanya na matamko wanayotoa, ni ishara kwamba Bunge linataka kuficha maovu au udhaifu wa mhimili huo au mihimili mingine inayowajibishwa na wabunge.

5.   Hatua hii ya kuzuia vikao vya Bunge kuonyeshwa moja kwa moja itakuwa inawachimbia kaburi la kisiasa wabunge kwani ndio wanaomulikwa kwa majibu ya maswali wanayoulizwa na hatua wanazochukua.

6.   Jukwaa la wahariri linaamini kwamba utaratibu huu unaoandaliwa sasa na Dk. Kashililah ni wa kidikteta na ni mbaya kuliko udikteta wowote uliowahi kutokea hapa nchini kwa miaka yote ya uhuru wa Tanzania.

7.   Kwa hatua hii uongozi wa Bunge utakuwa umedhihirisha udhaifu usiomithilika ambao uongozi wa Bunge uliopita uliuondoa kwa kuweka misingi na kanuni za uwazi na uwajibikaji. Ni kwa sura ya nje, harakati hizi za uongozi wa sasa wa Bunge zinaonekana kama hatua za kufuta yaliyofanywa na uongozi wa Bunge la tisa.

8.   Katika mazingira haya, tunaamini kwamba iwapo hili litatokea, jitihada ndogo za uwazi zilizokuwa zimefanywa na Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Jakaya Kikwete, zitafutika na kiumfanya raia aonekane mbele ya jumuiya ya kimataifa kuwa kiongozi dhalimu na dikteta asiyevumilia kukosolewa.

9.   Na kwa kuwa hili linatokea kueleka mwisho wa uongozi wake, ni dhahiri litakuwa limefuta mema mengi aliyotenda na kujivunia katika misingi ya uwazi na uwajibikaji.

10.                Kwa ujumla hatua hii itavifanya serikali na Bunge visiaminike kwa umma na itasababisha zogo na vurugu zisizomithilika kwani waliojifungia ndani watatoka na kusema hadharani kwa jinsi watakavyoona inafaa hivyo kuharibu kabisa mfumo wa taarifa za chombo hicho.

11.                Jukwaa linaamini kwamba njia halisi ya kurejesha amani Bungeni ni uongozi wa Bunge kutenda haki wa wabunge wote; maana hata vikao vyao visiporushwa moja kwa moja, vurugu hazitaisha iwapo wahusika hawataamini kwamba wanatendewa haki.

12.                Kuhusu suala la wabunge kulala bungeni na wakapigwa picha, tunasema magazeti na televisheni zinazofanya hivyo zinastahili kupongezwa badala ya kulaumiwa. Bungeni si mahala pa kusinzia, ni mahala pa kuchapa kazi. Wabunge wanaotaka kulala usingizi wabaki hotelini na si kulala kwenye ukumbi wa bunge.

HITIMISHO
1.           Watanzania wamepata fursa ya kuwafahamu wabunge wao baada ya utaratibu wa kurusha moja kwa moja mijadala ya wabunge kuanza miaka ya 2000. Kwa maana hiyo jaribio lolote la kuzuia matangazo hayo ni kuturejesha enzi za Bunge mazongwe na kadhia  ya kuficha habari ambapo hata barua za mialiko ziligongwa mihuri ya siri.

2.           Ndiyo maana tumesema hatua hii inakiuka misingi ya uhuru, uwazi na uwajibikaji wa vyombo vya umma na viongozi wa serikali. Ni mpango unaoweza kusababisha vurugu zitokanazo na kiu ya wananchi kujua kinachoendelea na kutumia taarifa potofu watakazozipata popote wanapojua na kwa staili wanayojua.

3.           Iwapo kuna kasoro katika Kanuni za Bunge zinazotokana na Sheria ya Haki, Wajibu na Mamlaka ya Bunge ya Mwaka 1988, basi kasoro hizo zirekebishwe na kuwabana wabunge  wanaozikiuka. Lakini hatukubaliana na mpango wa Bunge kuwaadhibu wananchi wasione kinachoendelea bungeni eti kwa lengo la kuwalinda wabunge.

4.           Mwisho tunasema nia ya kudhibiti (censorship), kuhariri na au kuzuia baadhi ya habari kutoka bungeni, kamwe Jukwaa la Wahariri halikubalini nayo na litaendelea kuipiga hadi hatua ya mwisho. Tunawataka wananchi watuunge mkono katika msimamo huu na sisi kama wahariri tutahakikisha tunachapisha maoni yao kwa kina kupinga suala hili.


Absalom Kibanda,
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF)
Dar es Salaam
Februari 15, 2013

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.