MTANGAZAJI

UPWEKE KWA WAHAMIAJI KUTOKA AFRIKA NCHINI MAREKANI

 


Wahamiaji kutoka Afrika wanaoishi Marekani wanakumbwa na changamoto kubwa ya upweke na kutengwa kijamii, licha ya kuongezeka kwa idadi yao kwa kasi kubwa katika miongo miwili iliyopita. 

Kwa mujibu wa ripoti ya Taasisi ya Sera ya Uhamiaji ya Marekani (mwaka 2022), zaidi ya watu milioni 2.75 waliozaliwa Afrika wanaishi Marekani, ikiwa ni ongezeko la zaidi ya asilimia 246 tangu mwaka 2000. Wahamiaji kutoka Nigeria wanaongoza kwa idadi, wakifuatwa na wale na wanaotoka Ethiopia, Misri, Ghana na Kenya.
Idadi kubwa ya wahamiaji hawa wako katika majimbo ya Texas, Maryland, New York na California. Hata hivyo, wengi wao husema wanakumbwa na upweke, hasa kutokana na ukosefu wa jamii pana za Kiafrika katika baadhi ya miji, tofauti za lugha, na kutopatikana kwa nyumba za ibada zinazowakilisha utamaduni wao. 
Utafiti wa kijamii uliochapishwa katika jarida la Frontiers in Sociology toleo la 2023 unaeleza kuwa wahamiaji wa Kiafrika wako katika hatari ya hali ya kutengwa kijamii na kisaikolojia kutokana na mabadiliko makubwa ya kitamaduni na kijamii wanayokutana nayo wanapowasili Marekani.
Taarifa zaidi kutoka Kituo cha Utafiti cha Pew (mwaka 2022) zinaonyesha kuwa asilimia 31 ya wahamiaji kutoka Afrika wana shahada ya chuo kikuu, lakini wengi wao bado hukumbwa na changamoto za ajira na kipato cha chini. 
Takriban asilimia 40 ya wahamiaji wa Kiafrika huishi chini ya mstari wa kipato cha wastani wa taifa, hali inayowalazimu kufanya kazi kwa muda mrefu na kuwanyima muda wa kushiriki katika shughuli za kijamii au ibada.
Upweke huu pia unaathiri kizazi cha pili cha wahamiaji, ambapo vijana hukumbwa na mgongano wa kitamaduni kati ya maadili ya Kiafrika waliyopewa nyumbani na utamaduni wa Kimarekani wanaoukuta shuleni au mitaani. 
Kwa mujibu wa ripoti ya Kituo cha Watoto na Familia cha Chuo Kikuu cha Georgetown ( 2023), hali hii huongeza hisia za kujitenga na huzuni, na wakati mwingine husababisha msongo wa mawazo au wasiwasi wa kijamii.
Taasisi za dini ikiwemo makanisa na misikiti zimekuwa sehemu muhimu kwa baadhi ya wahamiaji kupata faraja na kuunganishwa kijamii, lakini si kila mhamiaji hupata taasisi inayoendana na tamaduni na lugha yake. Hali hii inawafanya baadhi yao kujisikia kutengwa kiimani na kihisia.
Mashirika ya kijamii nchini Marekani, ikiwemo Jumuiya ya Waafrika na Kituo cha Wakimbizi na Taasisi ya Wahamiaji inayotoa Elimu na Huduma za Kisheria  yanatoa wito kwa serikali kuweka mikakati ya kusaidia ujumuishaji wa wahamiaji wa Kiafrika. Mapendekezo yao ni pamoja na kuanzisha huduma za afya ya akili zinazozingatia tamaduni za Kiafrika, kuimarisha usaidizi wa kisheria, na kuweka mazingira ya ajira jumuishi yanayowaruhusu wahamiaji kushiriki kikamilifu katika jamii bila ubaguzi.
Kwa ujumla, Hali ya maisha ya upweke inayoathiri wahamiaji kutoka Afrika nchini Marekani ni suala la kijamii, kiakili na kibinadamu linalohitaji mshikamano wa pamoja kutoka kwa jamii ya Marekani na jumuiya za kimataifa.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.