MTANGAZAJI

VITUO VINGI VYA AFYA NCHINI TANZANIA HAVINA DAWA ZA MALARIA

 
 
Asilimia 26 ya vituo 5,080 vya matibabu vya Serikali vilivyo katika mikoa 22 Tanzania Bara, havina dawa za aina yoyote za ngazi ya kwanza za kutibu malaria na kwinini ambayo hutumika kwa watu wenye malaria sugu.

Ngazi ya kwanza ya tiba ya malaria ni dawa mseto (ALu) na kwa wastani matumizi ya dawa za ALu nchini ni dozi milioni 1.3 kwa mwezi, ikimaananisha kuwa na dozi takribani 15,600,000 kwa mwaka.

Hata hivyo, taarifa zilizo katika ripoti ya Global Fund (kupitia ripoti za AMFm) Januari 1,2012 mpaka Januari 17, 2013 Tanzania iliagiza na kupokea dozi 4,917,780 kwa sekta ya umma kupitia Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kwa awamu nne kwa mwaka.

Dawa za kukabiliana na malaria hutolewa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kupitia mradi wa msonge unaoratibiwa na Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria (NMCP) ukifadhiliwa na wafadhili mbalimbali, hususan Global Fund, Mfuko wa Ufadhili wa Rais wa Marekani (PMI-USAID), Benki ya Dunia na wahisani wengine.

Kwa mujibu wa taarifa zilizo kwenye mtandao unaopokea taarifa za kila siku za uwepo wa dawa za malaria katika vituo vya serikali (SMS for Life) vingi ya vituo hivyo havijapokea dawa kwa siku hata 369.

Taarifa zilizotolewa na shirika lisilo la serikali linalofanya kazi ya kuboresha utawala bora, uwazi na uwajibikaji katika Sekta ya Afya na Ukimwi nchini (SIKIKA)katika mkutano na wahariri uliofanyika Dar es Salaam jana, zilisema uhaba huo wa dawa umekuwa ukitofautiana baina ya mikoa na wilaya.

Mkurugenzi wa Sikika, Irenei Kiria alisema uhaba uliopo na asilimia kwenye mabano ni Mwanza (57%), Ruvuma (53%), Mara (46%), Kigoma (43%), Shinyanga (42%) na Tabora (41%). Aliitaja yenye asilimia ndogo kuwa ni Dodoma asilimia 3, Singida 4%, Manyara 6% na Kilimanjaro asilimia 10.

Takwimu za Utafiti wa Virusi vya Ukimwi na Malaria nchini kwa mwaka 2007/8 maambukizi ya malaria mikoani, Mwanza inaonekana kuwa na maambukizi kwa asilimia 31 ukifuatiwa na Ruvuma 24%, Mara 30%, Kigoma 20% na Shinyanga 30% na ndio mikoa inayoongoza kwa uhaba mkubwa wa dawa hizo.

Aidha, alisema hali ni mbaya katika wilaya kwenye mikoa yenye uhaba mkubwa. "Katika mkoa wa Mwanza, wilaya ya Ukerewe imeripotiwa kuwa na uhaba wa ALu kwa asilimia 88 katika vituo vyake vya huduma, ikifuatiwa na Sengerema 80%, Geita 70% na Misungwi 65%," alisema Kiria.

Kiria alisema uhaba wa dawa umejitokeza sana kwa kipindi kirefu sasa ingawa kumekuwa na mipango na miongozo thabiti ya kupambana na malaria.

"Katika nchi ambayo kila mwaka watu kati ya  60,000 na 80,000 hufariki dunia kwa malaria, upungufu huu ni hatari kubwa," alisema Kiria na kuongeza kwamba taarifa za sasa za upungufu ni za Januari 28.

Wahariri wakichangia mada hiyo waliungana na Sikika kuitaka Serikali ikomeshe uhaba sugu na kuishiwa dawa mara kwa mara, kufanya ununuzi wa mwaka mzima ili kuwa na dozi milioni 15.6 na kuhakikisha kuwa na dawa za ziada za kutosha angalau kila baada ya miezi sita.

Walisema hilo linawezekana kwa kuwa fedha zinazofadhili mradi huo zinatoka nje na wakati huo huo serikali lazima itafute rasilimali pesa za kutosha  ili kununua dawa za ALu.

Sikika imekuwa ikifuatilia uwepo wa ALu kupitia mfumo wa Serikali kwa miaka miwili sasa na kugundua upungufu huo ambao unaonekana hakuna mtu anayeufanyia haraka kuuondoa.
 
Chanzo:Wavuti

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.