MTANGAZAJI

POLISI WAENDELEA KUELEZA CHANZO CHA KIFO CHA KAMANDA LIBERATUS BARLOW

Aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Liberatus Barlow wakati uhai wakeMwelekeo wa upelelezi wa mauaji ya aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow umebadilika na sasa tukio hilo linahusishwa na kisasi cha mapenzi na tayari mtu mmoja anayedaiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi Mwalimu Dorothy Moses kutiwa mbaroni na polisi.Awali, ilidaiwa kwamba Kamanda Barlow ambaye aliuawa kwa risasi usiku wa kuamkia Jumamosi muda mfupi baada ya kumfikisha mwalimu huyo nyumbani kwake, alivamiwa na majambazi.Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, DCI, Robert Manumba alithibitisha jana kukamatwa kwa mtu huyo (jina tulihifadhi) akisema: “Ni kweli mtu mmoja amekamatwa, lakini kwa sasa siwezi kuzungumzia kwa kina kuhusu suala hilo kwa sababu bado tunamhoji na  tunaendelea na uchunguzi. Tutakapokamilisha, tutatoa taarifa.”

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Lily Matola pia alithibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo. Hata hivyo, alisema amesikia habari hizo kwa kuwa yuko safarini kwenda mkoani Kilimanjaro kwenye mazishi ya kamanda huyo... “Hayo nimesikia, lakini kwa sasa sipo Mwanza hivyo siwezi kuzungumzia lolote.”

Habari za uhakika kutoka ndani ya Jeshi la Polisi, zinaeleza kwamba upelelezi wa mauaji hayo umefanikiwa kwa hatua kubwa na kwamba mtu huyo alikamatwa Dar es Salaam baada ya kuwekewa mtego na makachero waliopo katika timu ya uchunguzi na alisafirishwa hadi Mwanza ambako anashikiliwa na jeshi hilo.

Ilielezwa kuwa mtu huyo alikamatwa kutokana na kuwapo kwa taarifa za siri za kiitelejensia kutoka kwa watu mbalimbali.

“Kuna hali imefunguka na imesaidia sana. Inaonyesha kwamba Dorothy alikuwa na uhusiano na mtu huyu ambaye alikuwa akifika nyumbani kwake, kama mumewe na watu wanajua jambo hili,” alieleza mmoja wa askari polisi ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.
Alisema kwamba uchunguzi wa awali unaonyesha kwamba uamuzi wa mwalimu huyo kusitisha uhusiano wa mapenzi na mtu huyo huenda ndicho chanzo cha mauaji hayo lengo likiwa ni kumshawishi Dorothy kurejesha uhusiano.
“Mimi natambua kwamba huyu jamaa na Dorothy walikuwa na uhusiano na inajulikana mjini kuwa hata mke wa mtuhumiwa anatambua jambo hilo kwani walishagombana siku moja mjini na hata katika msiba nyumbani kwao na mtuhumiwa,” alisema mama mmoja (jina tunalo), aliyejitambulisha kama mmoja wa marafiki wa karibu wa Dorothy.


Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Kitangiri (jina tunalo), anasema amekuwa akimfahamu mtuhumiwa aliyekamatwa kama baba mwenye nyumba hiyo na kila mara amekuwa akimkuta hapo nyumbani wakati wa kujisomea na wanafunzi wenzake.

“Mimi ninamfahamu kama baba wa rafiki yangu na nimewahi kumkuta wakati wa kujisomea hapo nyumbani na watoto wa nyumba hiyo.”

Dorothy ambaye ametajwa kuwa mjane, ni Mwalimu katika Shule ya Msingi Nyamagana na tangu kufariki kwa mumewe Ofisa wa zamani wa TRA, Modest Lyimo mwaka 1997.
“Watu wote wanajua kwamba mtuhumiwa alikuwa akitembea na huyo mwalimu, wameonekana mara nyingi wakiwa muziki,” alieleza mmoja wa ndugu wa karibu wa mke wa mtuhumiwa.

Hili ni tukio la tatu mkoani Mwanza kutokea kwa ofisa wa polisi kuuawa. Katika tukio la awali lililotokea mwaka 1987, askari aliyetambulika kwa jina la Inspekta Gamba aliuawa kwa risasi na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi eneo la Nyakato na katika tukio la pili mwaka 1997, aliyekuwa Mkuu wa Kituo cha Kati ASP Mahende aliuawa kwa kupigwa risasi eneo la Bugando saa nne usiku alipokuwa akifuatilia majambazi waliokuwa wakijitayarisha kuvamia.
 Chanzo:Gazeti la Mwananchi

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.