MCHUNGAJI BLASIOUS RUGURI KUSTAAFU DISEMBA 2026
Divisheni ya Afrika Mashariki na Kati ya Kanisa la Waadventista wa Sabato (ECD) imetoa taarifa ya rasmi ya kustaafu kwa Kiongozi wa Kanisa hilo katika ukanda huo wenye nchi 11, Mch Blasious Ruguri ambapo atastaafu rasmi Disemba 31, 2026.
Taarifa hiyo rasmi ya kustaafu kwa Ruguri imetolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa ECD, Mch Christopher Ungani ikipewa kichwa cha habari "Taarifa kuhusu kustaafu kwa Mch Blasious Ruguri" imetolewa wakati kukiwa na taarifa isiyo rasmi iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuanzia alhamisi ikidai mchungaji huyo aliwaaga rasmi wafanyakazi wa ECD kutoka kwenye nafasi hiyo.
Kwa mujibu wa ECD, Mchakato wa kupitisha uongozi mpya utafuata taratibu za Kanisa la Waadventista Ulimwenguni ambapo waumini wameombwa kuendelea kuombea divisheni, viongozi wake, na mchakato mzima wa mpito wa uongozi.
Mchungaji Blacious Ruguri, aliyezaliwa 1958 nchini Kenya, amekuwa mchungaji wa Kanisa la Waadventista wa Sabato kwa takribani miaka 44.
Alisoma Thiolojia katika Chuo Kikuu cha Bugema mwanzoni mwa miaka ya 1980, kisha akapata Shahada ya Uzamili wa Huduma ya Uchungaji na Uzamivu katika Chuo Kikuu cha Andrews nchini Marekani. Rekodi za Kanisa la Waadventista wa Sabato pia zinaonyesha kuwa amewahi kutunukiwa Shahada ya Heshima katika Uongozi wa Kanisa iliyotolewa na Chuo Kikuu Waadventista cha Afrika (AUA) kutokana na mchango wake katika elimu na utawala wa kanisa .
Alianza huduma mwaka 1982, akitumikia katika nafasi ya mchungaji wa mtaa kabla ya kuongoza Idara ya Vijana na Uwakili kati ya 1986–1995, Kuanzia 1995–2003, alihudumu kwa nafasi ya Mkurugenzi wa idara hizo katika Divisheni ya Afrika Mashariki (EAD) makao makuu yakiwa Harare, Zimbabwe wakati huo. Mwaka 2003, alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa ECD, nafasi aliyoitumikia hadi 2010.
Katika Mkutano Mkuu wa Kanisa la Waadventista wa Sabato Ulimwenguni wa 2010, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa ECD, Divisheni inayosimamia nchi za Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda, Burundi, Ethiopia, Eritrea, Somalia, Sudan Kusini, Djibouti na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zenye zaidi ya waumini wa kanisa hilo wapatao milioni 5 kwa takwimu za 2025. Alichaguliwa tena katika nafasi hiyo mwaka 2015, 2020, na 2025 ambapo alipaswa ashike nafasi hiyo hadi 2030.

.png)
Post a Comment