MTANGAZAJI

MCHUNGAJI MWADVENTISTA MSTAAFU ATAJWA UCHUNGUZI VIFO VYA WAKE WAWILI.


Maafisa wa upelelezi katika jimbo la Kentucky na Oregon nchini Marekani wanachunguza vifo vya wanawake wawili vilivyotokea miongo kadhaa iliyopita, wote wakiwa wameolewa kwa nyakati tofauti na John Thomas Bridges, mchungaji mstaafu wa Waadventista wa Sabato mwenye umri wa miaka 86 anayeishi Sheldon, Missouri, kwa mujibu na taarifa za tovuti ya People na Newsweek. Polisi wa Gresham, Oregon, wamemtaja Bridges kuwa mshukiwa katika kifo cha mwaka 1993 cha mke wake wa pili, Astrid Bridges. 

Hajakamatwa wala kushtakiwa kwa kosa lolote, na Newsweek iliripoti Alhamisi kwamba Bridges hakujibu mara moja maombi ya kutoa maoni.

Astrid alifariki mwaka 1993 katika tukio lililoonekana awali kuwa ajali, ambapo mke wa kwanza wa Bridges, Joyce “Mable” Bridges, alifariki huko Louisville, Kentucky, mwaka 1972. Vifo vyote viwili baadaye vilitambuliwa kuwa mauaji.

 Polisi wa Louisville walisema mwezi uliopita kwamba kesi ya Joyce bado iko wazi na inaendelea, na wanatafuta taarifa kutoka kwa yeyote aliyeifahamu familia ya Bridges. Polisi wa Gresham pia wamekuwa wakishirikiana na wachunguzi wa Louisville wakati idara hizo mbili zinapochunguza kesi hizo. Newsweek, ikinukuu NBC News, iliripoti kwamba wake wanne wa Bridges wamefariki tangu 1972, ingawa uchunguzi wa sasa unahusu mke wa kwanza na wa pili.

Kumbukumbu za Waadventista zinaonyesha kwamba Bridges alitumia miongo kadhaa akifanya kazi katika kanisa hilo. Aliwekewa mikono ya uchungaji huko Kentucky mwaka 1970 na baadaye akahudumu akiwa mchungaji, mhubiri, mwalimu, na mkurugenzi wa idara za Konferensi. 

Mwaka 1986, Jarida la Southwestern Union Record liliripoti kwamba Bridges na Astrid walijiunga na Kanisa la Waadventista la Gentry huko Arkansas baada ya kuhudumu katika Konferensi ya Kaskazini mwa New England, likibainisha kwamba tayari alikuwa amekamilisha miaka 22 ya utumishi kwa kanisa. 

Kumbukumbu za kanisa pia zinaonyesha kwamba alihudumu katika nafasi za uchungaji na idara huko Oregon, Montana, Arkansas,Louisiana, na maeneo mengine. Uchunguzi bado unaendelea, na mamlaka hazijatangaza mashtaka yoyote dhidi ya Bridges.


No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.